Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah (Subhaanah) ameeleza juu ya kiumbe mjuzi kabisa kuliko wote katika zama zake, naye ni msemezwa Wake, muokolewa Wake na mtakasifu katika ardhi, ya kwamba alimuomba Mola Wake (Ta´aala) apate kumuona. Mola Wake (Tabaarak wa Ta´ala) akamwambia:

لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي ۚ فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا

“Hutoniona! Lakini tazama jabali. Likitulia mahali pake, basi utaniona.” Basi Mola wako alipojidhihirisha katika jabali, akalifanya livurugike kuwa vumbi.” (07:143)

Dalili [juu ya kuonekana kwa Allaah] katika Aayah hii zinaweza kuwakilishwa kwa njia nyingi:

Mosi: Isifikiriwe kwa mtu ambaye ni msemezwa wa Mwingi wa Rahmah na ambaye ni Mtume Wake mtukufu ya kwamba anaweza kuthubutu kumuomba Mola Wake kitu kisichojuzu. Hii ni batili kubwa kabisa na ni kitu kisichowezekana kabisa [kufikiria hivyo]. Lakini vifaranga vya yonani [wagiriki], wafuasi wa ´Abdullaah bin Sabaa´ na wafuasi wa Fir´awn wanaonelea [alivyofanya] ni kitu kilicho katika ngazi ya kumuomba [Mola Wake] ale, anywe, alale na mfano wa hayo katika mambo ambayo Allaah (Ta´ala) ametakasika nayo. Ni ajabu iliyoje kuona wafuasi wa ´Abdullaah bin Sabaa´, wafuasi wa waabudu Moto, washirikina wenye kuabudu masanamu, vifaranga vya Jahmiyyah na Fir´awn wakawa ni wajuzi zaidi juu ya Allaah kuliko Muusa mwana wa ´Imraan, juu ya mambo ambayo ni muhali Kwake, ambalo lilikuwa la wajibu kwake na kumtakasa kuliko kukubwa zaidi kuliko yeye [Muusa]!

Pili: Allaah (Subaanah) hakumkaripia Muusa. Lau ingelikuwa ni kitu kisichowezekana kabisa basi angelimkemea. Kwa ajili hii wakati Ibraahiym Khaliyl alipomuomba Mola Wake amuonyeshe namna anavyohuisha maiti hakumkaripia, wakati ´Iysaa alipomuomba Mola Wake kuteremsha chakula kutoka mbinguni hakumkatalia maombi yake na wakati Nuuh alipomuomba kumuokoa mtoto wake Akamkemea maombi yake na kumwambia:

إِنِّي أَعِظُكَ أَن تَكُونَ مِنَ الْجَاهِلِين قَالَ رَبِّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ أَنْ أَسْأَلَكَ مَا لَيْسَ لِي بِهِ عِلْمٌ ۖ وَإِلَّا تَغْفِرْ لِي وَتَرْحَمْنِي أَكُن مِّنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika mimi najikinga Kwako kukuomba yale nisiyo na elimu nayo. Na Usiponisamehe na ukanirehemu, basi nitakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (11:46-47)

Tatu: Alimjibu kwa kumwambia:

لَن تَرَانِي

“(Lan) hutoniona!”

Hakumwambia:

“(Laa) hunioni!”

“Mimi sionekani.”

“Haijuzu Kwangu kuonekana.”

Tofauti kati ya majibu mawili hayo ni kitu kiko wazi kwa yule mwenye kuzingatia.

Hii ni dalili yenye kufahamisha kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ataonekana. Lakini hata hivyo Muusa hawezi kumuona katika dunia hii kutokana na udhaifu wa maumbile ya mwanaadamu juu ya kumuona Allaah (Ta´ala). Hili linawekwa wazi zaidi na nukta ya nne:

Nne: Amesema (Ta´ala):

وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي

“Lakini tazama jabali. Likitulia mahali pake, basi utaniona.”

Akamjuza ya kwamba mlima, pamoja na nguvu zake hauwezi kuthibiti Atapojidhihirisha kwenye mlima huo katika dunia hii. Vipi basi kwa mwanaadamu dhaifu ambaye ameumbwa kutokana na udhaifu.

Tano: Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni Muweza wa kujidhihirisha kwenye mlima na ukabaki mahala pake hali ya ni wenye kutulia. Hili ni jambo lisiloshindikana kwa uwezo Wake. Bila ya shaka ni jambo linalowezekana. Amefungamanisha hilo na kuonekana. Lau ingelikuwa ni jambo muhali kwa dhati yake kabisa basi asingefungamanisha hilo na kitu ambacho ni chenye kuwezekana kwa dhati yake. Jengine ni kwamba lau kuonekana kwa Allaah ingelikuwa ni kitu ambacho ni muhali kabisa, basi ingelistahiki kusemwa:

“Likitulia mahali pake hapo ndio naweza kula, kunywa na kulala.”

Mambo mawili hayo kwa mujibu wenu mnaonelea kuwa ni sawa!

Sita: Amesema (Subhanaanahu wa Ta´ala):

فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا

“Basi Mola wako alipojidhihirisha katika jabali, akalifanya livurugike kuwa vumbi.”

Hii ni dalili ya wazi kabisa juu ya kujuzu kuonekana kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Ikiwa inajuzu Kwake kujionyeshe kwenye mlima, ambao ni kiumbe kisichokuwa na uhai wa dhahiri, kisichokuwa na thawabu wala adhabu, vipi atakosa kujionyesha kwa Manabii Wake, Mitume Wake na mawalii Wake Peponi? Hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akamfahamisha Muusa ya kwamba ikiwa mlima hutoweza kuthibiti kwa kumuona hapa duniani basi mwanaadamu ni mdhaifu zaidi.

Sita: Mola Wake (Subaahanahu wa Ta´ala) alimzungumzisha, akamnong´oneza na akamwita. Ambaye kumejuzu Kwake kuzungumza na kuongea na kumsikilizisha mzungumzishwaji maneno akaweza kuyasikia Maneno Yake wakiwa pamoja, bila ya kuwepo kizuizi chochote, basi kuonekana Kwake ni kitu cha aula zaidi juu ya kujuzu kwake. Kwa ajili hii hakutimii kwa mtu kupinga kuonekana kwa Allaah mpaka kutimie kupinga pia kuzungumza. Mapote haya yamekutana kati ya kupinga mambo mawili:

1- Wamepinga juu ya Allaah kumzungumzisha yeyote.

2- Wamepinga kwa mtu yeyote kuweza kumuona.

Kwa ajili hii ndio maana baada ya Muusa kusikia Maneno Yake ndio akawa amemuomba pia aweze kumuona. Akamjuza Mtume Wake juu ya kujuzu kumuona kwa kitendo cha kuweza kuzungumza Naye. Hakumweleza kuwa hilo ni muhali Kwake kutokea. Lakini akamuonesha kuwa alichomuomba hakiwezekani kama jinsi mlima pia haukuweza.

Kuhusiana na Kauli Yake:

لَن تَرَانِي

“(Lan) hutoniona!” (07:143)

Inafahamisha juu ya ukanushaji wa huko mbeleni na haitolei dalili juu ya ukanushaji wa milele hata kama ukanushaji utaambatanishwa na umilele. Vipi iweje pale ambapo ukanushaji haukuambatanishwa na umilele! Amesema (Ta´ala):

وَلَن يَتَمَنَّوْهُ أَبَدًا بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ

“Na (Lan) hawatoyatamani [hayo mauti] hata siku moja kutokana na yaliyoyatanguliza mikono yao.” (02:95)

Pamoja na maneno Yake (Ta´ala):

وَنَادَوْا يَا مَالِكُ لِيَقْضِ عَلَيْنَا رَبُّكَ

“Wataita: “Ee Maalik [mlinzi wa Moto]! Na atumalize [tufe] Mola wako.” (43:77)

MAELEZO

Aayah hii ambayo Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) ametolea dalili kwayo juu ya kujuzu kuonekana kwa Allaah Peponi kwa njia sita au saba wameshikamana nayo wale wenye kupinga kuonekana kwa Allaah. Mu´tazilah, Khawaarij na wengine wameshikamana nayo miongoni mwa wale wenye kupinga kuonekana kwa Allaah (´Azza wa Jall) Aakhirah. Wamesema kuwa Amesema kumwambia Muusa:

لَن تَرَانِي

“(Lan) hutoniona!”

Wanaonelea kuwa ukanushaji huu wa “lan” ni wa milele. Huu ni uongo kuizulia lugha na Qur-aan. Wanayodai sio sahihi. Kwa hivyo maimamu wa Ahl-us-Sunnah kupitia Aayah hii wakatoa dalili juu ya kujuzu kuonekana kwa Allaah kwa njia alizotaja Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah). Ni neema ya ueelewa uliyoje! Ninaapa kwa Allaah huu ndio uelewa. Tunamuomba Allaah atupe uelewa sote katika dini Yake.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Bayaan wa al-Idhwaah li ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy Ru´yati Allaahi yaum al-Qiyaamah, uk. 11-14
  • Imechapishwa: 27/08/2020