Ni wajibu kuyatolea zakaah mapambo ya dhahabu na fedha

Swali: Ni yepi maoni ya mwisho kuhusu zakaah ya mapambo yanayovaliwa ya dhahabu na fedha? Nini wanachomaanisha wanazuoni wanaposema kuwa zakaah ni kukua na kuongezeka? Ni kipi kile kiwango kilchowekwa?

Jibu: Ni wajibu kuyatolea zakaah mapambo yanayovaliwa ya dhahabu na fedha. Dalili ya kwamba ni wajibu kuyatolea zakaah mapambo ya dhahabu na fedha ni kule kuenea kwa dalili pasi na upambanuzi. Jengine ni kwamba zipo Hadiyth maalum zinazotilia nguvu zakaah ya vito. Baadhi yake zimetajwa katika “Buluugh-ul-Maraam”.

Kuhusu kwamba zakaah ni ule ukuaji na kuongezeka ndio utambulisho wake katika lugha. Mali haihitaji kuongezeka ili iwe ni wajibu kutolewa zakaah. Kwa hiyo kama mtu yuko na pesa za kutosha na zikafikia kile kiwango kinachowajibisha kutoa zakaah na wakati huohuo amezihifadhi ili aweze kununua kwa mfano nyumba au matumizi, basi anawajibika kuzitolea zakaah hata kama hazitoongezeka wala kuzidi.

Ikiwa mwanamke hana pesa za kutolea zakaah vito vyake, basi anawajibika kuuza mapambo yake kwa kiasi cha zakaah anayotakiwa kutoa. Anaweza pia kutoa mapambo kwa kiasi cha zakaah anayopaswa kutoa. Ikiwa vito vyake vitapungua kile kiwango kinachowajibika kutoa zakaah basi havotilea zakaah. Aidha hakuna tofauti ikiwa mapambo hayo anayavaa siku zote au anayavaa katika minasaba fulani tu.

Kuhusu kile kiwango ambacho inawajibika kutoa zakaah, kiwango cha dhahabu ni gramu 85 na kiwango cha fedha ni gramu 595.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (18/137-138)
  • Imechapishwa: 04/05/2026