Swali: Ni nani ambaye halazimiki kufunga?

Jibu:

1 – Mwendawazimu.

2 –  Aliyepoteza akili.

3 – Mtoto ambaye hajabaleghe.

Kuhusu mwenye hedhi na mwenye damu ya uzazi hawalazimiki kufunga. Lakini haifai kwao kufunga katika Ramadhaan na wakati mwingine wanapokuwa na hedhi na nifasi. Wanalazimika kulipa yale masiku ya Ramadhaan waliyokula.

Kuhusu mgonjwa na msafiri inafaa kwao ima kufunga na kuacha kufunga katika Ramadhaan. Ingawa kula ndio bora zaidi. Aidha wanalazimika kulipa endapo watakula ndani ya Ramadhaan. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

”Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Lakini ikiwa maradhi ya mgonjwa hayatarajiwi kupona kwa mujibu wa ushahidi wa madaktari waaminifu, basi mgonjwa huyo halazimiki kufunga wala kulipa kwa baadaye. Atalazimika kulisha masikini juu ya kila siku. Ni nusu ya pishi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya chakula kinacholiwa katika nchi. Kiwango chake ni takriban 1,5 kg. Vivyo hivyo watu wazima na vikongwe wasioweza kufunga watapaswa kulisha nusu pishi ya chakula kinacholiwa katika nchi. Baada ya hapo hawatofunga wala kulipa. Inafaa kutoa kafara juu ya Ramadhaan yote mara moja mwanzoni, mwishoni au katikati mwa mwezi kumpa fakiri mmoja au wengi. Vivyo hivyo hali ya mjamzito na mnyonyeshaji swawm ikiwa ngumu kwao watakula na kulipa baadaye kama anavofanya mgonjwa.

[1] 02:185

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/من-لا-يجب-عليه-الصوم
  • Imechapishwa: 22/03/2023