Ni lini nasaha zinakuwa kwa siri na lini zinakuwa waziwazi?

Swali: Ni lini nasaha zinakuwa kwa siri na lini zinakuwa hadharani?

Jibu: Anayetoa nasaha afanyie kazi kile chenye manufaa zaidi. Akiona kuwa manufaa zaidi ni kutoa nasaha kwa siri basi afanye hivo na akiona manufaa zaidi ni kunasihi hadharani basi afanye hivo. Lakini kama dhambi imefanywa kwa siri ni lazima nasaha iwe kwa siri. Ikiwa anajua dhambi ya ndugu yake aliyoifanya kwa siri basi amnasihi kwa siri na asimuanike. Amnasihi baina yake na yeye. Ama ikiwa dhambi imefanywa waziwazi wakaiona watu kwa mfano mtu amesimama katika mkusanyiko wa watu na akanywa pombe, basi amkemee papohapo. Mfano mwingine mtu amesimama akaagiza pombe na yeye yuko mahali hapo au ribaa, basi anatakiwa kumwambia kwamba haifai kufanya hivo. Kuhusu dhambi unayoijua kutoka kwa ndugu yako ambapo ukajua kuwa ndugu yako anakunywa pombe au unajua kuwa anakula ribaa, basi unatakiwa kumnasihi kati yako wewe na yeye kwa siri na kumweleza kuwa umefikiwa na khabari kadhaa. Lakini kama anafanya maovu hadharani kwenye kikao na wewe au watu wengine wanaona maovu hayo basi unatakiwa kumkataza. Ukinyamaza hiyo maana yake ni kuwa umekubaliana na batili. Kama tuko katika kikao ambapo kukadhihiri unywaji pombe basi unatakiwa kukemea kama una uwezo wa kufanya hivo. Vivyo hivyo kukidhihiri maovu mengine kama ya usengenyi basi unatakiwa kumnasihi ndugu yako na kumweleza kuwa haijuzu kusengenya na maasi mengine ya waziwazi kama hayo. Ikiwa uko na elimu basi unatakiwa kuyakataza kwa sababu hayo ni maovu ya waziwazi. Usiyanyamazie kwa ajili ya kudhihirisha na kulingania katika haki.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majallat-ul-Iswlaah nr. 17-241 tarehe 23/06/1993 M
  • Imechapishwa: 07/11/2022