Ni ipi Sunnah wakati wa kulisindikiza jeneza na wakati wa kuzika?

Swali: Ni ipi hukumu ya mwenye kusema “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah! Uso wa Allaah ndio wenye kudumu!” wakati wa kuliandama jeneza kwa sauti ya juu na wakati wa kuzika wanasema “Ee Mwingi wa Rahmah! Ee Mwingi wa Rahmah!”? Ni ipi Sunnah wakati wa kusindikiza jeneza na wakati wa kumzika maiti?

Jibu: Ni Bid´ah. Hapana shaka ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba hakuna atayebaki isipokuwa Yeye pekee. Hata hivyo ni Bid´ah kusema yale yote yaliyotajwa kwenye swali. Kila ´ibaadah ambayo haikufanywa na Salaf ni Bid´ah. Vilevile ni Bid´ah kusema “Ee Mwingi wa Rahmah! Ee Mwingi wa Rahmah!” wakati wa kuzika.

Sunnah wakati wa kulisindikiza jeneza ni mtu kuzingatia na kufikiria mwisho wake. Hivi sasa anaenda kwenye jeneza, kesho jeneza hili litambeba yeye. Ayazingatie matendo yake na hali yake.

Kuhusu wakati wa kuzika, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa akimaliza kuzika alikuwa akisema:

“Muombeeni msamaha ndugu yenu na mumtakie uthabiti, hakika hivi sasa ataulizwa.”[1]

Haya ndio yamewekwa katika Shari´ah.

[1] Abu Daawuud (3221).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/165)
  • Imechapishwa: 24/08/2021