Ni ipi hukumu ya wale wanaoyaomba wafu ndani ya makaburi?

Swali 2: Yale yanayofanywa na baadhi ya wajinga pambizoni na makaburi katika kuwaomba wafu, kuwataka msaada, kuwataka uombezi, kuwaomba nusura dhidi ya maadui au kuwaomba uokozi. Ni ipi hukumu yake? Kwa sababu mambo haya yanafanyika katika miji mingi.

Jibu: Kwa jina la Allaah na himdi zote njema ni stahiki ya Allaah.

Kitendo hichi ni katika shirki kubwa. Nayo ndio shirki ya washirikina wa mwanzo katika Quraysh na wengineo. Walikuwa wakimwabudu al-Laat, al-´Uzza, Manaat na mizimu na masanamu mengi. Wakiyaomba uokozi na wakiyaomba msaada dhidi ya maadui zao. Kama alivosema Abu Sufyaan siku ya Uhud:

”Sisi tuko na al-´Uzza na nyinyi hamna al-´Uzza.”

Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaambia Maswahabah:

”Mwambieni Allaah ndiye Mola wetu na nyinyi hamna mola.”

Abu Sufyaan akasema:

”Habal yuko juu.”

Ni sanamu ambalo Quraysh walikuwa wakiliabudu Makkah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Mjibuni.” Wakasema: ”Tumwambie nini, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Semeni ”Allaah yuko juu na ni mtukufu zaidi.”

Makusudio ni kwamba kuwaomba wafu, masanamu, miti, mawe na viumbe vyenginevyo na kuwataka msaada, kuwaomba nusura, kuwachinjia, kuwawekea nadhiri na kuwafanyia Twawaaf yote hayo ni shirki kubwa. Kwa sababu matendo yote hayo ni katika kumwabudu mwengine asiyekuwa Allaah na ni katika matendo ya washirikina waliotangulia na waliokuja baadaye. Hivyo ni lazima kutahadhari kutokamana na hayo na kutubu kwa Allaah kutokamana na mambo hayo. Ni wajibu kwa wanachuoni na walinganizi kumnasihi anayefanya mambo hayo, amjuze, amwelekeze na amwekee wazi kwamba mambo hayo ni shirki iliokuwa inafanywa na washirikina wa kale ambao Allaah amesema juu yao:

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[1]

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[2]

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha bila shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda.”[3]

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

“Hakika yule atakayemshirikisha Allaah, basi hakika Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni motoni – na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kuwanusuru.”[4]

Amesema (´Azza wa Jall) juu yake akimzungumzisha Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Mwenye kufa ilihali anamwomba Allaah mshirika ataingia Motoni.”

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Haki ya Allaah juu ya waja wamwabudu Yeye na wala wasimshirikishe na chochote.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Yeyote mwenye kukutana na Allaah hali ya kuwa hamshirikishi na chochote ataingia Peponi na yeyote mwenye kukutana Naye hali ya kuwa anamshirikisha na chochote ataingia Motoni.”

Ameipokea Muslim katika ”as-Swahiyh” yake.

Zipo Aayah na Hadiyth nyingi kwa maana hii.

[1] 10:18

[2] 04:48

[3] 06:88

[4] 05:72

[5] 39:65

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Akhtwaau fiyl-´Aqiydah, uk. 7-8
  • Imechapishwa: 05/08/2020