Ni ipi hukumu ya mwenye kuacha swalah tatu za ijumaa kwa uzembe?

Swali: Ni ipi hukumu ya mwenye kuacha swalah tatu za ijumaa kwa uzembe?

Jibu: Ijumaa ni neema ya Allaah juu yetu. Ni miongoni mwa mambo ambayo Allaah ameyafanya kuwa maalum juu ya Ummah huu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akawapoteza kutokamana nayo mayahudi na manaswara. Kwa hivyo ni neema ya Allaah kwa Ummah huu. Tunatakiwa kumshukuru Allaah juu ya neema hii, kumsifu kwayo, kumhimidi kwa kutuchagulia nayo, kutufanyia maalum na kutuneemesha kwa fadhilah kubwa ndani yake. Haifai kwa muislamu mwenye imani ya kweli kukosa swalah ya ijumaa. Haijuzu kwake kufanya hivo. Kukosa na kuipuuza ni jambo la khatari. Imepokelewa katika Hadiyth isemayo:

“Yeyote anayeacha ijumaa tatu kwa uzembe basi Allaah atapiga muhuri juu ya moyo wake.”

Hii ndio adhabu yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema juu ya daraja ya mimbari yake:

“Wakome watu wanaosikia wito siku ya ijumaa kisha hawauendei au Allaah atapiga muhuri juu nyoyo zao kisha watakuwa miongoni mwa waghafilikaji.”

Hili ni janga kubwa kupigwa muhuri juu ya moyo. Tunamwomba Allaah usalama na afya. Haifai kwa muislamu kuipuuza. Bali afurahie, amhimidi Allaah kuidiriki na kushiriki ndani yake ili aweze kupata fadhilah zake kuu.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalish-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.mufti.af.org.sa/ar/content/من-ترك-ثلاث-جمع-تهاوناً-وكسلاً
  • Imechapishwa: 11/06/2022