Ni ipi hukumu ya kuyajengea makaburi mawe na kuandika juu yake?

Swali: Katika baadhi ya miji wanaweka kipande cha jiwe juu ya kaburi ambacho kinakuwa kimepanda kwa juu kiasi fulani. Baadhi ya wengine wanaandika kwenye jiwe hilo:

يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ ارْجِعِي إِلَى رَبِّكِ رَاضِيَةً مَّرْضِيَّةً فَادْخُلِي فِي عِبَادِي وَادْخُلِي جَنَّتِي

“Ee nafsi iliyotua! Rejea kwa Mola wako hali ya kuwa umeridhika na mwenye kuridhiwa. Basi ingia katika waja Wangu na ingia kwenye Pepo Yangu.”[1]

Kisha wanaandika jina la maiti. Ni ipi hukumu ya hilo?

Jibu: Haya ni maovu na ni haramu. Ni lazima liondoshwe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuyajengea makaburi, kukaa juu yake, kuyatia chokaa[2] au kuyaandika[3]. Alimtuma (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) ayasazawazishe makaburi yote yaliyoinuliwa yaliyo tofauti ili yawe kama makaburi mengine.

Ni wajibu kwa watu hawa kuondosha lile jiwe waliloweka. Baadhi ya wanachuoni wanasema kuwa maiti anaudhika na yale madhambi yanayofanywa kwenye kaburi lake. Ni dhambi. Kwa muqtadha wa maneno ya wanachuoni ni kwamba maiti anaudhika kwa yale yaliyowekwa kwenye kaburi lake. Kwa hiyo hakikisha kuyatendea kazi na uwaeleze kuwa ni wajibu kuliondosha. Ni neema kutoka kwa Allaah kwao na juu ya maiti wao kuliondosha. Wasipofanya hivo ni wajibu kwa wale wenye majukumu makaburini kuliondosha.

Ni kipi kilichowajuza kuwa nafsi imefika katika utulivu? Hawajui. Je, kuna ambaye anajua kuwa mtu huyu amekufa juu ya Tawhiyd na imani? Sisi tunaangalia udhahiri, lakini kuhusu mambo ya Aakhirah hatujui yalivyo.

[1] 89:27-30

[2] Muslim (970).

[3] at-Tirmidhiy (1052) ambaye amesema kuwa ni nzuri na Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/188-189)
  • Imechapishwa: 25/08/2021