Ni ipi hukumu ya kuweka majani na nyasi juu ya kaburi?

Swali: Ni ipi hukumu ya kuweka majani au nyasi juu ya kaburi kwa kuzingatia ya kwamba kuna ambao wanadai kuwa nyasi hii inazuia udongo kushuka chini ndani ya kaburi?

Jibu: Katika baadhi ya miji ni lazima waweke majani ya limau au majani mengine mfano wa hayo. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokataza kukata majani na miti Makkah, Ibn ´Abbaas akasema: “Isipokuwa majani ya mlimau kwa kuwa yanatumiwa kwa nyumba na makaburi yao.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Isipokuwa majani ya mlimau.”[1]

Ikiwa kuna haja ya kuyaweka kati ya kokoto [zinazowekwa juu ya mwanandani] haina neno.

Ama kuweka majani juu ya kaburi, sio katika uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kilichopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwamba alipita karibu na makaburi mawili na akasema:

“Hakika hawa wanaadhibiwa, na hawaadhibiwi kwa kitu kikubwa. Ama mmoja wao alikuwa hakijikingi na cheche za mkojo na mwengine alikuwa akieneza uvumi.” Baada ya hapo akachukua kuti na akaligawa mara mbili na akaweka kwenye kila kaburi kuti moja. Wakasema: “Mtume wa Allaah! Kwa nini umefanya hivo?” Akasema: “Pengine wakakhafifishiwa adhabu midhali bado [makuti hayo] ni kijani.”[2]

Hili ni jambo maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kuwa alijua kuwa watu walio ndani ya makaburi haya mawili wanaadhibiwa. Leo hii mtu kufanya hivo ni kwamba anamdhania vibaya yule maiti kwa sababu anafikiria kuwa anaadhibiwa.

[1] al-Bukhaariy (1349) na Muslim (1353).

[2] al-Bukhaariy (218) na Muslim (292)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/193-194)
  • Imechapishwa: 25/08/2021