Ni ipi hukumu ya kula daku wakati muadhini anaadhini?

Swali: Je, inafaa kuendelea kula daku na huku muadhini anaadhini adhaana ya pili au ajizuilie?

Jibu: Hapana kunahitajia upambanuzi. Ikiwa muadhini ameadhini baada ya kuingia alfajiri na wewe ukajua kuwa kumeshapambazuka, basi itakulazimu kujizuilia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Adhaana ya Bilaal isikuzuilieni na daku yenu. Kwani hakika yeye anaadhini usiku. Hivyo basi, kuleni na kunyweni mpaka aadhini Ibn Umm Maktuum.”

Msingi wa hili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِۖ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku.”[1]

Akijua kuwa kumeshapambazuka alfajiri – hata kama hawajaadhini – kama ambaye yuko jangwani au mfano wake akiona kuingia kwa alfajiri basi anapaswa kujizuilia hata kama hajasikia adhaana.

Lakini ikiwa muadhini anaadhini mapema au anatilia shaka kama adhaana yake inaafikiana na alfajiri au hapana, basi inafaa kwake kula na kunywa mpaka awe na uhakika wa kuingia kwa alfajiri. Anaweza kufanya hivo ima kwa saa zinazotambulika ambazo zimewekwa sawa kwamba alfajiri imekwishaingia au kwa adhaana ya mwaminifu ambaye anajua kuwa huadhini baada ya kuingia alfajiri. Katika hali ya adhaana ya kwanza inafaa kwake kula na kunywa kile kilichomo mkononi mwake kwa sababu adhaana haina uhakika kuwa ni baada ya kuingia alfajiri.

[1] 02:187

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (15/282)
  • Imechapishwa: 19/04/2022