Ni ipi hukumu ya “Chakula cha Ramadhaan”?

Swali: Ni ipi hukumu ya “chakula cha jioni cha Ramadhaan” kinachohusiana na kuchinja kichinjwa kimoja au viwili na kualika watu. Kitendo hichi kinachukuliwa ni wajibu kwa watu wengi. Kwa mtazamo wao wanaonelea kuwa swadaqah zingine zote si sahihi. Mara nyingi hakuna faida ya chakula hichi. Watu wengi wanakuja tu kwa ajili ya kutaka kumpaka mafuta mwalikaji. Inaweza kutokea katika usiku mmoja kukawa sherehe mbili. Je, kitendo hichi ni cha sawa? Kuna njia nyingine ya faida?

Jibu: Mwaliko huu ambao vilevile unaitwa “Chakula cha wazazi wawili” kinaweza kupitika kwa njia mbili:

1 – Mchinjaji akaitakidi kuwa atajikurubisha kwa Allaah kwa kichinjwa hichi. Bi maana mchinjaji akaonelea kuwa kichinjwa kwa dhati yake ni ´ibaadah kama inavyokuwa katika ´Iyd-ul-Adhwhaa. Hii ni Bid´ah. Kichinjwa ni ´ibaadah katika matukio yaliyowekwa katika Shari´ah kama Udhhiyah, ´Aqiyqah na hajj.

2 – Mchinjaji akawa amechinja sio kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah bali ni kwa ajili ya nyama. Badala ya kununua nyama sokoni akaonelea wacha achinje nyumbani kwake. Hili halina neno. Lakini haitakiwi kufanya israfu. Mfano wa hilo ni mtu akachinja zaidi ya haja na akawaalika watu wengi ambao wanakuja tu kwa ajili ya kutaka kuwapaka watu mafuta. Baadaye kukaja kubaki chakula kingi ambacho kitaharibika bila ya faida.

Naonelea kuwa badala yake mtu atoe pesa, nguo, chakula na mfano wa hayo kuwapa mafukara. Yafanyike kwa sababu ya faida mbili: 1- Yanawanufaisha mafukara.

2 – Ni salama zaidi kwa kutumbukia katika israfu na ni rahisi kwa mwalikaji na mwalikwaji.

Hapo kabla watu walikuwa katika hali ya shida. Kuwapikia watu chakula ilikuwa ni jambo lenye kuwaathiri wengi. Matajiri walikuwa wakiwatengenezea chakula na kuwaalika watu kwenye chakula hicho. Leo hali imebadilika na himdi zote ni za Allaah na kwa hiyo wasilinganishwe na kipindi kile.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/237-238)
  • Imechapishwa: 02/09/2021