Elimu ya wanachuoni na wanafunzi inafungua njia ya nguvu ya dini. Mwanachuoni, au mwanafunzi, anakuwa ni mwenye dini ya nguvu. Hababaishwi na shaytwaan isipokuwa akitaka Allaah (Jalla wa ´Alaa).

Mwanafunzi imani yake inakuwa ni yenye nguvu kwa kuwa anaamini kwa dalili.

Mwanafunzi matendo yake yanakuwa na nguvu kwa kuwa anaabudu kutokamana na ujuzi wa namna alivyoabudu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Pindi mwanafunzi anapoabudu anatambua ni dalili zipi anazotumia katika ´ibaadah yake. Kwa hivyo inakuwa undani na uinje wake umefungamana na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati anaposwali, anapoabudu, anapouunga uhusiano, anapolingania, anapopambana, anapoamrisha mema na kukataza maovu. Anayafanya yote hayo kwa elimu na ujuzi. Tofauti na yule anayeyafanya mambo haya pasi na elimu. Anakuwa sio mwenye kufungamana na mwongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wala hamkumbuki Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na matendo ya Salaf katika suala hilo.

Baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah mwanafunzi amefungamana na maimamu wa Uislamu. Wakati anapotenda anatambua kuwa maoni fulani ni ya Imaam Ahmad, ash-Shaafi´iy, Sa´iyd bin Jubayr, Imaam Maalik, Ibn Taymiyyah, Ibn Hazm na wengineo. Wakati wote anakuwa na wanachuoni hawa vigogo katika fikira zake. Anakuwa na mawasiliano yenye kuendelea na wanachuoni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wewe utakuwa pamoja na yule unayempenda.”

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muhadhara: Fadhwl-ul-´Ilm wa Ahlihi wa Swifatuhum
  • Imechapishwa: 12/03/2017