Haja kubwa ya wanafunzi hii leo

Elimu na masomo ni katika ´ibaadah kubwa kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Wanachuoni wengi wamezingatia kuisoma elimu ndio kitendo chema zaidi cha Sunnah ambacho mja anaweza kujishughulisha nacho. Kueneza elimu yenye manufaa yenye kutoka katika Qur-aan, Sunnah na yale waliyobainisha maimamu waaminifu wa Qur-aan na Sunnah ni mapambano katika njia ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) na ni kitendo ambacho kinamchukiza shaytwaan na maadui wa dini. Huu ndio uhakika wa mambo. Wanachuoni, haijalishi ni wakati na sehemu gani, ndio warithi wa Mitume. Hii ina maana kuwa wao ndio wasimamizi wa dini. Kila ambavyo elimu inavyozidi ndivyo kheri inavyozidi na kila ambavyo elimu inavyopungua ndivyo ujinga na shari inavyozidi kuongezeka.

Hakika hii leo tuna haja kubwa ya wanafunzi wataowafunza waislamu ulimwenguni dini yao. Watu wa leo wana haja ya watu ambao watawabainishia haki, Tawhiyd sahihi, ´Aqiydah safi, maana ya kufuata Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), hukumu za Shari´ah, njia ya nguvu yao katika dini na njia ya mfumo wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hili linahitajia idadi kubwa ya wanafunzi sawa wa ndani na nje ya nchi hii. Watu wanahitajia sana wanafunzi wataowafunza.

Katika Fiqh kuna kanuni inayosema kuwa njia ina hukumu moja kama lengo. Ikiwa lengo lina fadhila, hukumu na matunda kama haya basi njia za kuifikia, bidii za kuiendea na kuisambaza zina hukumu moja kama lengo lenyewe kutokamana na ule uwajibu, kuichuma na kuieneza. Kwa hivyo mtu anapewa thawabu kwa njia hiyo ikiwa inaafikiana na Shari´ah kama ambavyo anapewa thawabu kwa lile lengo linaloafikiana na Shari´ah. Wanachuoni wa misingi wanasema:

”Kile ambacho wajibu haitimii isipokuwa kwacho basi nacho ni wajibu.”

Njia inafuata lile lengo; ikiwa lengo ni wajibu basi nji zake pia itakuwa ni wajibu kwa njia ya hukumu na thawabu. Ikiwa lengo limependekezwa basi njia zake pia zitakuwa zimependekezwa. Ikiwa lengo ni haramu basi njia zake pia zitakuwa ni haramu mpaka pale dalili zitapothibitisha kinyume chake.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muhadhara: Fadhwl-ul-´Ilm wa Ahlihi wa Swifatuhum http://saleh.af.org.sa/sites/default/files/101.mp3
  • Imechapishwa: 12/03/2017