Swali: Unasemaje kuhusu mwanamke na kulingania katika dini ya Allaah?

Jibu: Yeye ni kama mwanaume ambapo anawajibika kulingania katika dini ya Allaah na kuamrisha mema na kukataza maovu. Dalili za Qur-aan na Sunnah zinafahamisha hivo. Maneno ya wanachuoni yako wazi juu ya hilo. Ni wajibu kwake kulingania katika dini ya Allaah na aamrishe mema na akataze maovu kwa adabu za Kishari´ah zinazotakikana kwa mwanaume pia. Pamoja na hayo ni wajibu kwake asikome kulingania kwa Allaah kutokana na kukata tamaa na uchache wa subira kwa sababu kwa kuwepo baadhi ya watu wenye kumtweza, kumtukana na kumfanyia maskhara. Ni wajibu kwake kustahamili na kuvumilia hata kama ataona kutoka kwa watu ambayo yanaweza kuchukuliwa kama maskhara na istihzai.

Ni lazima kwake kuzingatia jambo lingine; nalo ni kwamba anatakiwa kuwa mfano mzuri katika usafi na kujisitiri kutokamana na wanaume ambao ni ajinabi na ajiepushe kutokamana na mchanganyiko. Kulingania kwake kuambatane na kujichunga na kila kile anachokikemea. Akiwalingania wanaume basi awalinganie ilihali ni mwenye kujisitiri na asikae faragha na yeyote katika wao. Akiwalingania wanawake basi awalinganie kwa hekima na awe msafi katika tabia na historia yake ili wasimpinge na wasimpuuze ni kwa nini hakuanza na nafsi yake mwenyewe.

Ni wajibu kwake vilevile kujiepusha na mavazi ambayo huenda wengine wakatiwa katika mtihani kwa sababu yake. Anatakiwa ajitenge mbali na kila sababu inayopelekea katika fitina kama vile kuonyesha mapambo na sauti legevu, mambo ambayo anayakemea. Anachotakiwa ni kutilia umuhimu kulingania katika dini ya Allaah kwa njia isiyodhuru dini na sifa zake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/240)
  • Imechapishwa: 16/07/2017