Namna hii mali inakuwa mtihani kwa mwanaadamu

Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“… kama jinsi mtu anavyoweza kumuomba kitu ambacho kina fitina kwake. Hakika ataadhibiwa kwa hilo lau ataitikiwa na kuwekwa Motoni lau ikiwa Allaah Hatomsamehe kama jinsi mtu anavyoweza kumuomba Allaah kitu ambacho kitakuwa ni fitina kwake. Kama jinsi Tha´labah alivomuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amuombee kuwa na mali nyingi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkataza hilo mara kwa mara, hakuacha kufanya hivyo mpaka akamuombea Du´aa na hiyo ndio ikawa ni sababu kwake ya kutokuwa na furaha duniani na Aakhirah.”

Huyu ni Tha´labah bin Haatwib au Ibn Abiy Haatwib. Alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumuomba amuombee kwa Allaah Amruzuku mali. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkataza na kumwambia “Kidogo unachokiweza ni bora kuliko kingi usichokiweza”. Akakariri kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuashiria aachane na suala hili, kwa kuwa mali hii inaweza kumfitinisha. Akamng´ang´ania Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kila wakati mpaka akawa amemuombea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah Akamruzuku zizi la wanyama. Mwanzoni alikuwa anaswali na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kila wakati. Wanyama hawa wakamshughulisha na akawa haswali na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa Ijumaa tu. Wanyama wakazidi kuwa wengi na akawa ni mwenye kulazimika kuwafuga nje ya mji, hivyo akawa haswali pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) si Ijumaa wala mkusanyiko, Jamaa´ah. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotuma wakusanyaji Zakaah waende kuleta Zakaah, akawaambia “Niacheni, hiyo ni kodi, Jizyah. Nendeni”. Wakaenda kwa wengine na kuleta Zakaah na wakampitia tena, akawa amewapa kitu kwa kutenzwa nguvu na huku akiitakidi kuwa ni Jizyah. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Akamuadhibu kwa mali hii. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtahadharisha kutokana na fitina yake lakini akawa ameng´ang´ania hili na kumlilia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hiyo ikawa ni fitina kwake. Mtu anaweza kupewa kitu ambacho ni fitina kwake. Mtu aridhie kwa Allaah kwa kile ambacho kinamtosheleza tu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Iqtidhwaa’-is-Swiraat al-Mustaqiym (05) http://www.alfawzan.af.org.sa/node/2247
  • Imechapishwa: 05/05/2015