Mwenye kunyoa ndevu zake kinasihi kichinjwa chake katika ´Iyd-ul-Adhwhaa?

Swali: Mwenye kunyoa ndevu zake kinasihi kichinjwa chake katika ´Iyd-ul-Adhwhaa?

Jibu: Nasaha zangu kwa watu hawa wamche Allaah (´Azza wa Jall). Ni mamoja wamekusudia kuchinja au hawakukusudia. Ni lazima kwao kumcha Allaah na watekeleze amri ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Tofautianeni na washirikina na fugeni ndevu na punguzeni masharubu.”

Wanapaswa kutambua kwamba kufuga ndevu ni katika uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuzinyoa ni katika uongofu wa washirikina. Iwapo tutamuuliza ambaye anamwamini Allaah na Mtume wake kama anatanguliza mwongozo wa washirikina juu ya mwongozo wa kiongozi wa Mitume, jibu litakuwa hapana. Akiwa anasema kuwa hatangulizi mwongozo wa washirikina hata siku moja, ni kwa nini basi asichukue maazimio na akamcha Allaah?

Kwa ajili hii utawaona baadhi ya watu ni wenye kupupia kuswali swalah ya mkusanyiko, kufunga masiku meupe, kufunga swawm ya Nabii Daawuud, wakitoa swadaqah, ni mtu mwema na umbile zuri, lakini licha ya haya yote amepewa mtihani wa kunyoa ndevu. Hivyo kitendo hicho cha kunyoa ndevu kinakuwa ni upungufu katika tabia na dini yake. Kwa hivyo ni lazima kumcha Allaah (´Azza wa Jall).

Pengine kujizuia kwake kunyoa ndevu zake katika masiku kumi ya mwanzo ya Dhul-Hijjah ikawa ni sababu ya kujizuia maishani. Kwani kitendo hicho kinamsaidia. Kwa sababu kubakiza ndevu kwa muda wa siku kumi ambapo hazinyoi kutakuwa na athari yenye kuonekana wazi. Baada ya hapo inakuwa ni wepesi kwake kuzifuga na kutozinyoa.

Lakini baya zaidi kuliko hayo ni kwamba baadhi ya watu wanasema kuwa hawatochinja katika ´Iyd-ul-Adhwhaa kwa sababu eti wakinuia kuchinja kutawazuia kunyoa ndevu. Tunamwomba Allaah ulinzi kutokamana na kitendo hichi! Anaacha jambo la kheri kwa sababu ya kufanya maovu. Hili ni kosa kubwa. Katika hali hii tunamwambia kwamba achinje ijapo atamwasi Allaah kwa kunyo ndevu. Kuchinja Udhhiyah ni kitu kimoja na kunyoa ndevu ni kitu kingine.

Kadhalika napenda kuzindua yale wanayofikiri baadhi ya watu kwamba mwanamke akichanua nywele zake ndani ya masiku haya kumi basi kichinjwa chake cha Udhhiyah hakisihi. Hili pia ni kosa na si sahihi. Mwanamke kama amekusudia kuchinja katika ´Iyd-ul-Adhwhaa basi inafaa kwake kuchanua nywele zake lakini hata hivyo kwa utaratibu. Kukidondoka unywele bila ridhaa yake hakuna dhambi juu yake. Na ikiwa anachelea kwamba haiwezekani kuchanua pasi na kudondoka kitu basi asichanue. Lakini azioshe kwa maji, azibonye na kuzifanyia usafi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (25/147-150)
  • Imechapishwa: 27/07/2020