Mwanamke anapata ujira wa ´Umrah akikaa kumdhukuru Allaah baada ya Fajr mpaka jua kuchomoza?

Swali: Je, mwanamke ni kama mwanaume kuhusiana na Sunnah ya Rawaatib, Witr, Dhuhaa na kukaa msikitini baada ya al-Fajr mpaka jua lichomoze, bi maana na yeye akakaa katika mkeka wake? Tunaomba utuwekee wazi.

Jibu: Msingi ni kwamba mwanaume na mwanamke wako sawa sawa katika hukumu za Kishari´ah. Isipokuwa yale mambo ambayo dalili zimeonesha kuwa ni maalum kwa wanaume, katika hali hii itakuwa ni jambo maalum kwao. Au [dalili zimeonesha kuwa] ni maalum kwa wanawake, katika hali hii itakuwa ni maalum kwa wanawake. Mfano wa hili ni swalah ya mkusanyiko. Dalili zimeonesha kuwa ni jambo maalum kwa wanaume. Wao ndio ambao inawalazimu swalah ya mkusanyiko na kwamba waswali misikitini. Ama kuhusu wanawake swalah ya mkusanyiko haiwalazimu, si msikitini wala nyumbani kwake, bali kuswali nyumbani kwake ni bora kuliko kuhudhuria mkusanyiko pamoja na wanaume. Kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiwakataze wajakazi wa Allaah na Nyumba za Allaah na nyumba zao ni bora kwao.”

Sentisi hii ya mwisho, hata kama haiko katika al-Bukhaariy na Muslim, lakini ni sahihi. Nyumba zao ni bora kwao.

Kwa jili hii tunasema ya kwamba mwanamke ni kama mwanaume katika hukumu zote. Ikiwa ni msafiri inampasa kufanya kama yale yanayompasa kufanya mwanaume, bi maana hatakiwi kuswali Raatibah ya Dhuhr, Maghrib na ´Ishaa lakini Sunnah zingine azifanye. Atafanya yale yanayofanya mwanaume.

Kuhusiana na yeye kukaa kwenye mkeka wake nyumbani mpaka jua lichomoze na aswali Rak´ah mbili ili aweze kupata ujira kama wa aliyefanya ´Umrah na Hajj, kama ilivyokuja katika Hadiyth ambayo wanachuoni wametofautiana juu ya usahihi wake, hapati ujira huo. Kwa kuwa Hadiyth inasema:

“Mwenye kuswali Subh katika mkusanyiko kisha akakaa… “

Mwanamke sio katika wale wanaoswali Subh katika mkusanyiko. Akiswali nyumbani kwake hapati ujira huu. Hata hivyo yuko katika kheri ikiwa atakaa na kumdhukuru Allaah, kuleta Tasbiyh, Tahliyl na kusoma Qur-aan mpaka jua likachomoza. Halafu baada ya jua kuchomoza akaswali kiasi na anavyotaka, yuko katika kheri.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kanda “Liqaa´aatu Ramadhwaaniyyah”, sehemu ya 03
  • Imechapishwa: 23/09/2020