Mwanafunzi anayechanganyika na Hizbiyyuun kwa miaka mingi

Swali 05: Baadhi ya wanafunzi wanaandamana na baadhi ya wale ambao wameathirika na mifumo ya Hizbiyyah, kama vile al-Ikhwaan al-Muslimuun na Jamaa´at-ut-Tabliygh, wanaketi nao na wanahudhuria mikusanyiko na harakati zao. Wanafanya hivo kwa miaka mingi. Hali bado ni ileile hakubadilika kitu. Je, ni sahihi kufanya hivo? Ni upi mfumo wa Salaf juu ya jambo hili ambalo linawatatiza wengi ambao wanadai kuwa wanafata mfumo wa Salaf hii leo?

Jibu: Inanisikitisha kuona jambo hili linawatatiza watu ambao wanaishi katika nchi hii na vitabu vya Salaf vimejaa. Msimamo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya Ahl-ul-Bid´ah uko wazi kabisa kama jua. Nashangazwa kuona jambo hili linawatatiza watu ambao wanajinasibisha na mfumo wa Salaf.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha kukaa na Ahl-ul-Bid´ah  na waovu kwa ujumla. Salaf wametahadharisha jambo hili. Wale wanaokwenda kinyume na matahadharisho haya wanajiweka kwenye khatari na kupotea. Mtume mkarimu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha kukaa na watu waovu na akasema:

“Mfano wa rafiki mzuri na rafiki muovu ni kama muuza manukato na muhunzi. Muuza manukato ima atakupa au utapata kutoka kwake harufu nzuri. Kuhusu muhunzi ima ataunguza nguo yako au utapata harufu mbaya kutoka kwake.”[1]

Ni kwa nini hawachukui nasaha za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Kama hawakuathirika 100% basi wataathirika 90%. Hili khaswa kwa kuzingatia kwamba ametahadharisha nao mkweli na mwenye kusadikishwa na akaleta mfano huu mkubwa:

وَتِلْكَ الْأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ ۖ وَمَا يَعْقِلُهَا إِلَّا الْعَالِمُونَ

”Na hiyo ni mifano Tunawapigia watu. Lakini hawaifahamu isipokuwa wenye elimu.”[2]

Mwanachuoni anafaidika na mifano hii inayopigwa na Qur-aan au kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yote inatoka kwenye chemchem moja.

Hebu si wachukue nasaha za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Maimamu wa Uislamu, akiwemo al-Baghawiy na as-Swaabuuniy, wamesema kuwa kuna maafikiano juu ya kwamba wale Ahl-ul-Bid´ah waliopindukia wanatakiwa kukatwa, kuwatweza na kuwachukia. Kwa hiyo yule anayechanganyika nao, akatangamana nao na akasimama upande wao ataathirika na njia zao na fikira zao na atapewa mtihani wa kujikombakomba mpaka ufe moyo wake. Mara nyingi mtu kama huyo hupinda na akajiunga pamoja nao. Hayo yamewatokea wengi tuaowajua. Wao pia walikuwa wakijinasibisha na mfumo huu. Ni jambo la kusikitisha.

Nadharia inayosema kuwa tunakaa na Ahl-ul-Bid´ah na kuchukua haki kutoka kwao na kuacha batili ni nadharia ya khatari sana. Inapelekea katika matokeo mabaya. Hapana shaka kwamba kusoma vitabu vya Ahl-ul-Bid´ah na kukaa pamoja nao kunadhuru. Ni lazima kwa muislamu kuiheshimu dini yake na ahifadhi ´Aqiydah na mfumo huu. Allaah (Ta´ala) atasimamia jambo la yule ambaye hajali. Atakuja kupata matokeo yaliyozoeleka kwa yeye kutochukua nasaha za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na miongozo ya Salaf. Naapa kwa Allaah ya kwamba wao ni wenye hekima, wajuzi, wenye akili na watambuzi zaidi wa yale yanayopelekea katika mchanganyiko huu mbaya, ambao umetahadharishwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] Ahmad (4/404), al-Bukhaariy (2101) na Muslim (2628).

[2] 29:43

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kashf-us-Sitaar, uk. 14-16
  • Imechapishwa: 12/12/2023