Swali: Ni ipi hukumu kwa mtu ambaye watu wanakula kwake viapo vya utiifu? Je, inafaa kusema kuwa mtu kama huyo ni mzushi au ni katika matendo ya Khawaarij? Wakati mwingine ni kwamba kiapo hicho kinashurutisha mtu asioe wala asitoe talaka pasi na idhini ya kiongozi.

Jibu: Kiapo kilichowekwa katika Shari´ah na Uislamu na kikatambulika na wanazuoni na maimamu wa waislamu ni kile anachopewa mtawala wa waislamu. Kiapo kinahusu kumtii katika yale anayomtii Allaah, kupambana jihaad katika njia ya Allaah na kutekeleza adhabu za kidini kwa ajili ya kuihami dini na nchi. Kiapo hichi kilichotajwa katika swali hakitambuliwi na Ahl-u-Sunnah katika karne zote. Isipokuwa mtawala wa waislamu ndiye ambaye watu wanakula kwake kiapo. Kupitia kwake ndio waislamu wanakusanyika na kupitia kwake kunatekelezwa jambo la kumpwekesha Allaah, imani na jihaad.

Uislamu na waislamu wanajitenga mbali na viapo vya utiifu wanavyopewa wanazuoni, viongozi wa Suufiyyah na makhurafi. Viapo kama hivyo vimezuliwa na ni upotofu, khaswa ikiwa vitaenda mbali kufikia kwamba mtu hawezi kuoa, kutaliki wala kusafiri pasi na idhini. Pengine hata hawawezi kulala wala kuamka isipokuwa kwa idhini ya jitu hili. Mpotofu huyu amepewa jambo ambalo hakupewa hata Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hajui kuwa fulani ameoa isipokuwa baada ya kuoa na akaona kwake ishara za kuoa[1]. Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Jaabir:

”Umeoa, ee Jaabir?” Akajibu: ”Ndio.” Akasema: ”Bikira au mtumzima?” Akasema: ”Mtumzima.” Akasema: ”Ni kwa nini hukuoa bikira ambaye utacheza naye naye atacheza nawe, utamfanya kucheka naye akufanye kucheka?”[2]

Kwa msemo mwingine ni kwamba, Maswahabah walikuwa wakisafiri, wakioa na wakifanya biashara pasi na idhini ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakuwawekea sharti hiyo. Hayo hayakuingia katika kiapo alichopewa. Kitendo cha watu hawa kuwafanya watumwa kwa kuwashurutishia sharti hizi ni dalili kuwa ni wapotofu na wamezama katika Bid´ah. Kwa sharti hizi wanaupasua na kuufarikisha ummah, jambo ambalo limeharamishwa na Allaah:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

”Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.”[3]

إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ

“Hakika wale waliofarikisha dini yao na wakawa makundi makundi huna lolote kuhusiana na wao.”[4]

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَلَا تَكُونُوا مِنَ الْمُشْرِكِينَ مِنَ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا ۖ كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ

”… na simamisheni swalah; na wala msiwe miongoni mwa washirikina. Miongoni mwa wale walioitenganisha dini yaowakawa makundi makundi. Kila kundi kwa yaliyonayo linafurahia.”[5]

Dalili inayoonyesha kuwa ni mapote ni kwamba mfumo wa Jamaa´at-ut-Tabliygh unatofautiana na mfumo wa al-Ikhwaan al-Muslimuun, mfumo wa al-Ikhwaan al-Muslimuun unatofautiana na mfumo wa watu wa jihaad, na kadhalika, lakini kila mmoja anakula kiapo kwa kiongozi wake. Ni viapo vingapi vimewafanya waislamu wa leo kuwa watumwa na kuwafarikisha! Ni mambo mangapi ya ukambi na uchama, ushabiki na mapenzi ya kishaytwaan yametokea kwa sababu ya viapo hivi! Ni jambo analiona kila mtu mwenye busara.

[1] Maalik (1570), Ahmad (3/190), al-Bukhaariy (2049) na Muslim (1427).

[2] Ahmad (3/308), al-Bukhaariy (2097) na Muslim (715).

[3] 3:103

[4] 6:159

[5] 30:31-32

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kashf-us-Sitaar, uk. 112-114
  • Imechapishwa: 12/12/2023