Mtu ambaye haswali na wala hatoi zakaah

Swali: Kuna mtu kazi yake ni endelevu na kwa ajili hiyo haswali. Vilevile anayo hatoi zakaah kwa sababu ya wingi wa madeni yake na mahitaji yake. Ni ipi hukumu ya hayo?

Jibu: Suala hili limebeba mambo mawili ambapo moja wapo ni kuacha kuswali na jengine ni kuacha kutoa zakaah; mambo mawili hayo ndio nguzo mbili kubwa za Uislamu baada ya shahaadah.

Kuhusu swalah, hakuna yeyote anayepewa udhuru kuiacha kwa hali yoyote ile. Bali ni wajibu kwa muislamu kuswali ndani ya wakati wake, hata kama tutakadiria kuwa mtu atafukuzwa kazini kwake na kulazimika kwenda shambani na kuuza kuni na kuishi kwa kazi hiyo. Ni wajibu kwake kuswali ndani ya wakati wake. Wala haijuzu kwake kuichelewesha, kama wanavyofanya baadhi ya wajinga wanapotaka kwenda kulala ndio wanaswali swalah zote tano. Ni haramu kufanya hivo na ni dhambi kubwa, bali ni jambo linaweza kupelekea katika ukafiri.

Kuhusiana na zakaah, ni wajibu kwa mtu kutoa zakaah anapokuwa amehifadhi pesa na zikazungukiwa na mwaka mzima. Kitendo cha mtu kuhitajia pesa haina maana kwamba halazimiki kuitolea zakaah baada ya kutimia mwaka. Zakaah sio jambo kubwa na wala sio kiwango kikubwa cha pesa kinachotolewa. Inahusiana na 2.5%. Ni kitu kidogo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swadaqah haipunguzi mali.”[1]

Kinyume chake swadaqah inaziongezea baraka na ukuaji. Allaah anaweza kumfungulia mtu milango ya kheri kwa namna ambayo alikuwa haitarajii pale anapotekeleza yale ambayo Allaah amemuwajibishia juu ya mali yake. Kwa mujibu wa maoni yenye nguvu ni lazima kwa muislamu kuitolea zakaah mali yake yote alionayo baada ya kutimiza mwaka ijapokuwa yuko na deni. Lakini kuhusu ile pesa aliyoitumia au mtu akalipa deni lake kabla ya kukamilisha mwaka, pesa hiyo haitolewi zakaah.

[1] Muslim (2588), at-Tirmidhiy (2029) na Ahmad (2/235).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/46-47)
  • Imechapishwa: 17/06/2026