Swali: Inakuweje watu wa leo kupatwa na majini na watu wanajishughulisha na matabano na kupokea malipo juu ya kazi yao hiyo kwa kujengea hoja Hadiyth ya Abu Sa´iyd al-Khudriy?

Jibu: Hapana vibaya kupokea malipo juu ya matabano. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kitu ambacho kina haki zaidi ya kukichukulia malipo ni Kitabu cha Allaah.”[1]

Mfanya matabano ni kama daktari tofauti na msomaji ambaye anachukua malipo kwa ajili ya kusoma tu. Ni haramu kwa mtu kusoma Qur-aan kwa ajili ya kumwabudu Allaah na akapokea malipo kwa jambo hilo. Hata hivyo inafaa kwa mtu kuchukua malipo kwa ajili ya kuwasomea wengine kwa lengo la matibabu au kuwafundisha.

Kuhusiana na madai kwamba wanawasomea majini au kwamba majini wanawazungumzisha, ni jambo ambalo linahitaji kuthibitishwa. Hata hivyo si jambo la mbali kwamba majini wanawazungumzisha watu na kuwaambia wawe waislamu au makafiri. Nimewasikia baadhi ya wafanya matabano wakisema kuwa majini wanaowaingia watu wanasema kuwa ni waislamu lakini hawataki kutoka ndani ya watu hao kwa sababu wanawapenda. Wakati mwingine majini hao husema wazi kwamba ni mayahudi, manaswara, wabudha au makafiri wengine na hawataki kutoka nje.

Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) ameeleza kwamba mwalimu wake Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) alijiwa  na mtu ambaye ameingiwa na jini. Akaanza kumsomea mtu yule, lakini jini yule akakataa kutoka. Ndipo akampiga kipigo kikali. Ndipo jini yule, ambaye alikuwa mwanamke, akaanza kumzungumzisha. Mwanamke yule akasema kuwa anampenda. Ibn Taymiyyah akasema: “Lakini yeye hakupendi.” Mwanamke yule akasema: “Mimi nataka kuhiji naye.” Ndipo akamwambia: “Lakini yeye hataki kuhiji naye.” Ndipo akaanza kumpiga kwa nguvu kifuani na akachoka kwenye mkono. Baada ya muda fulani mwanamke yule akasema: “Natoka kwa ajili ya heshima ya Shaykh.” Ndipo akasema: “Usitoke kwa ajili ya heshima yangu; toka kwa ajili ya kumtii Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Ndipo mwanamke yule akatoka. Bwana yule akaamka na kustaajabu; ni kipi kilichomfanya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah kuja? Hakuhisi kipigo kile. Kwa sababu udhahiri ni kwamba kipigo kinampata bwana yule, lakini uhakika wa mambo kinapata yule jini.

[1] al-Bukhaariy (5737).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/39-40)
  • Imechapishwa: 17/06/2026