Msichana wa miezi sita amezikwa kwenye kaburi moja na mvulana wa miezi sita mimba iliyoporomoka

Swali: Msichana wa miezi sita amezikwa pamoja na mvulana wa miezi sita wa mimba iliyoporomoka. Je, inajuzu? Ikiwa haijuzu ni ipi hukumu ya wale waliowazika kwenye kaburi moja?

Jibu: Kilichowekwa katika Shari´ah ni kila maiti kuzikwa kwenye kaburi lake. Hii ndio ilikuwa desturi ya waislamu tokea wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka hii leo. Lakini kukiwa kuna haja ya kuwazika watu wawili au zaidi kwenye kaburi moja, haina neno. Imethibiti katika alBukhaariy ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwakusanya watu mashahidi wawili au watatu wa Uhud kwenye kaburi moja[1]. Kulikuwa kuna haja ya kufanya hivo.

Hivi sasa sio wajibu kumfukua msichana huyu na mimba hii iliyoharibika waliyozikwa kwenye kaburi moja. Muda umeshapita. Aliyewazika kwenye kaburi moja kwa sababu ya ujinga hana dhambi. Lakini kwa kila kitendo cha ´ibaadah na vyenginevyo inapaswa kwa mtu kutambua mipaka ya Allaah (´Azza wa Jall) juu ya kitendo hicho ili mtu asitumbukie katika dhambi.

[1] al-Bukhaariy (1345).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/214-215)
  • Imechapishwa: 01/09/2021