Swali: Ramadhaan iliyopita nilipatwa na baadhi ya maumivu na sikuweza kufunga. Hivyo nikala na nikamlazimisha mke wangu ambaye alikuwa akiandamana nami katika kipindi cha matibabu naye kula pia. Hivi sasa nataka kulisha chakula kwa sababu ya kushindwa kwangu kufunga. Je, yale niliyofanya juu ya mke wangu yanafaa? Je, inasihi kwangu kulisha chakula? Je, inafaa kwangu kumtolea chakula mke wangu kwa sababu ni mwenye kunyonyesha wakati wa sasa?

Jibu: Kuacha kwako kufunga kwa sababu ya maradhi ni kitu kilichoruhusiwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi atimize idadi katika masiku mengine.”[1]

Kuhusu kumlazimisha kwako mke wako kula kwa sababu ya wewe kuumwa sioni wajihi wake. Kwa sababu yeye sio mgonjwa, sio msafiri na sio miongoni mwa wale waliopewa udhuru. Umekosea kumlazimisha kula ilihali yeye sio miongoni mwa wale waliopewa udhuru. Lakini muda wa kuwa jambo limekwishatokea basi ni lazima kwa mke wako kulipa. Akiwa ameingilia na Ramadhaan nyingine kabla ya kulipa kwake ya kabla pasi na udhuru, basi sambamba na kulipa atatakiwa kulisha chakula kwa kila siku moja. Akiwa alikula kwa sababu ya kunyonyesha kwa sababu funga inamdhuru yeye na mtoto wake kwa kupungua maziwa, basi ni sahihi kula katika hali hii. Kwa sababu ataingia miongoni mwa wale waliopewa udhuru. Haitotosha kwake kulipa peke yake. Bali sambamba na kulipa atalazimika kulisha chakula kwa sababu aliacha kufunga kwa sababu ya kumyonyesha mtoto wake. Katika hali hiyo atalazimika kulipa pamoja na kulisha masikini kwa kila siku moja iliyompita.

[1] 02:185

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (02/412-413)
  • Imechapishwa: 17/03/2022