Swali: Je, ni lazima mwezi mwandamo uonekane kwa macho peke yake? Je, inafaa kuutazama kwa msaada wa darubini? Kama mnavotambua inawezekana kuhesabu mwezi mwandamo, lakini hata hivyo hesabu hizo za astronomia ni lazima ziwe zaidi ya saa saba. Anasema uwongo ambaye amesema kuwa ameuona kabla ya hapo?

Jibu: Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuwekea wazi kabisa pale aliposema:

“Fungeni mtakapouona na fungueni mtakapouona. Mkifunikwa na wingu basi hesabuni siku thelathini.”[1]

Ametuamrisha kufunga na kufungua wakati tunapoona mwezi mwandamo. Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fungeni mtakapouona na fungueni mtakapouona. Mkifunikwa na wingu basi ukadirieni.”[2]

Kimsingi ni kule kuuona. Hata hivyo hakuna neno kutumia msaada wa vifaa vya kuuona. Kuhusu hesabu za astronomia ni zenye kukataliwa kwa maafikiano ya waislamu. Hakuna mazingatio ya kuhesabu na pia haina uzito wowote, kitu ambacho waislamu wameafikiana kwacho. Hesabu za astronomia sio mategemezi katika kuingia mwezi mwandamo wala kumalizika kwa Ramadhaan. Wala kuingia kwa mwezi wa Dhul-Hijjah. Kwa sababu jambo hilo linaenda kinyume na Shari´ah. Hakika sisi tumeongozwa katika njia nyepesi, nayo ni kuuona kwa macho. Fungeni pale mnapouona na fungueni pale mnapouona. Hesabu za astronomia ni zenye kugongana, kutofautiana, isiyokuwa ya kawaida na pia ngumu kwa watu wengi, tofauti na uonekanaji ambao ni jambo liko wazi kabisa. Kwa ajili hiyo nchi yetu bado inaendelea kufanyia kazi Sunnah hii. Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye ametusahilishia kuafikiana na Shari´ah Yake na kufuata Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] al-Bukhaariy (1900) na Muslim (1080).

[2] al-Bukhaariy (1900) na Muslim (1080).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Fataawaas-Swiyaam, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 17/03/2022