Ahmad al-Ghumaariy amesema:

“Tambua kwamba Hadiyth zilizopokelewa juu ya watokaji ni zenye kufanana na Hadiyth za Khawaarij. Hata kama wote ni wenye kutoka katika dini (خوارج عن الدين) na wote ni mijibwa ya Motoni, kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), pamoja na hivo wamegawanyika mafungu mawili:

1 – Fungu la kwanza wanatambulika kwa jina hili. Wamesifiwa kuwa ni wenye kujikakama na kuchupa mpaka katika dini na kwamba mmoja wetu atazidharau swalah na swawm zake ukilinganisha na swalah na swawm zao.

2 – Fungu la pili ni wale wapotofu wa sasa (ملاحدة العصر). Wamesifiwa kuwa wapumbavu na vijana na kwamba alama zao ni kunyoa upara.

Pindi kulipozuka pembe ya shaytwaan huko Najd mwishoni mwa karne ya kumi na fitina yake ikaenea, basi wanachuoni wote walikuwa wakizitumia Hadiyth hizi juu yake na wafuasi wake, kwa sababu kulikuwa hakujazuka aina ya Khawaarij hawa hapo kabla.”[1]

Sita: Miongoni mwa maajabu ni kwamba amewathibitishia imani watu wa Misri na kwamba wao ndio kundi lililonusuriwa mpaka siku ya Qiyaamah. Sambamba na hilo amemtuhumu Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab kwamba ndiye pembe ya shaytwaan, kwamba ni mweneza fitina na kuwaita watu wa Najd kwamba ni “watu wenye pembe”. Hakika ni jambo lisilofichikana kwa kila mtu kwamba mambo ni kinyume.

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab alilingania kwa Allaah kwa njia timilifu kabisa. Allaah akabariki ulinganizi wake na kupitia yeye akaihuisha dini Yake baada ya kuchafuka. Kupitia yeye Akaieneza Sunnah katika kisiwa cha waarabu na maeneo kwengine, kuitokomeza Bid´ah na akaisafisha Najd kutokamana na mambo ya kipindi cha kikafiri. Vivyo hivyo ndivo walivyofanya watoto wake, wajukuu wake, wanafunzi  wake na wanachuoni huko Najd. Wote walikuwa katika njia ilionyooka na mfumo imara. Walikuwa wakilingania kwa Allaah kwa utambuzi na wakipambana na washirikina na wazushi. Vitabu vyao ni vyenye kutolea ushuhuda juu ya hayo.

Kuhusu watu wa Misri, tumekwishatangulia kutaja namna walivyopewa mtihani wa makaburi na kuwaomba wenye nayo na kuwaelekea katika vipindi vizito. Pia nimekwishataja namna Bid´ah, mambo ya ukhurafi na aina mbalimbali za maasi zilivyoenea kwao kwa kiwango kikubwa. Pia nimekwishataja namna walivyotupilia hukumu za Shari´ah nyuma ya migongo yao na badala yake kuchukua hukumu zilizotungwa na watu kutoka katika kipindi cha kikafiri. Wanashikamana na ujamaa na desturi za kikafiri katika mambo yao mengi. Pamoja na haya yote mtunzi anasema kuwa wako katika haki na kwamba wao ndio kundi lililonusuriwa na kwamba Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab yeye ndiye pembe ya shaytwaan mweneza fitina na kwamba watu wa Najd ndio pembe ya shaytwaan. Huku ni kuyapindua mambo. Mtunzi amefanana na wale ambao Allaah amesema juu yao:

أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَـٰهَهُ هَوَاهُ وَأَضَلَّهُ اللَّـهُ عَلَىٰ عِلْمٍ وَخَتَمَ عَلَىٰ سَمْعِهِ وَقَلْبِهِ وَجَعَلَ عَلَىٰ بَصَرِهِ غِشَاوَةً فَمَن يَهْدِيهِ مِن بَعْدِ اللَّـهِ ۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ

“Je, umemuona yule aliyejifanyia matamanio yake kuwa ndio mungu wake na Allaah akampotoa juu ya kuwa na elimu na akapiga muhuri juu ya masikio yake na moyo wake na akaweka kizibo juu ya macho yake? Basi nani atamwongoza baada ya Allaah? Ni kwa nini hamkumbuki?”[2]

[1] Mutwaabaqat-ul-Ikhtara´aat al-´Aswriyyah, uk. 76

[2] 45:23

  • Mhusika: ´Allaamah Hamuud bin ´Abdillaah at-Tuwayjiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Iydhwaah-ul-Mahajjah, uk. 140-141
  • Imechapishwa: 08/07/2020