Misikiti mitatu ambayo ndio bora pasi na shaka haikupambwa. Kuna Hadiyth nyingi zinazotahadharisha mapambo kama haya. Pamoja na hivo hayakuwanufaisha kitu wale wajengaji wa misikiti ingawa jambo hilo litafanyika katika hesabu ya wale wenye kujitolea. Wale wajengaji wanatumbukia katika makosa mawili. Kosa la kwanza ndio lile ambalo tunalizungumzia, nalo ni kwenda kinyume na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye katika Hadiyth nyingi amekataza kuipamba misikiti. Moja katika Hadiyth hizo ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Sikuamrishwa kuipamba misikiti.”

Bi maana kwa kuipaka rangi na kuipamba. Kinachoashiria katika hilo ni msimuliaji wa Hadiyth ambaye ni ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameiwekea taaliki Hadiyth hiyo kwa kusema:

“Hakika mtakuja kuipamba kama walivyopamba mayahudi na wakristo.”

Ni kama kwamba maneno haya ya ´Abdullaah bin ´Abbaas yametoka katika chemchem ya ujumbe wa kinabii kwa sababu ni yenye kuafikiana na hali ya waislamu hii leo. Hii leo kutokana na kupindukia kwenye mapambo tunakaribia kutoona tofauti yoyote kati ya msikiti na kanisa. Maneno ya Ibn ´Abbaas yanaweza kuwa yake mwenyewe lakini yenye hukumu ya maneno ya Mtume na pia yanaweza kuwa yametokana na Ijtihaad yake mwenyewe ambayo imejengeka juu ya Hadiyth zilizokuja kwa njia ya ujumla kama mfano wa:

“Mtafuata nyayo za wale waliokuwa kabla yenu hatua kwa hatua, shibiri kwa shibiri, mpaka wakiingia shimo la mburukenge nanyi mtaingia. Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Unamaanisha mayahudi na manaswara?” Akasema: “Kina nani wengine?”

Kadhalika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza na kutahadharisha mapambo haya pale aliposema:

“Saa haitosimama mpaka watu wafakhirishane kwa misikiti.”

Huu ndio ukweli wa mambo unaosikitisha wa hali ilivyo hii leo kwa sababu unakwenda kinyume na mafunzo ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Tatizo jingine ni kwamba ambaye anachangia kujenga msikiti amekwenda kinyume na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuhusu wale wanaokusanya michango wanakosea kwa sababu wanaiweka katika yale mambo ambayo hayakuwekwa katika Shari´ah.

Kwa ajili hiyo mimi namtahadharisha kila yule ambaye anajitolea kushiriki kujenga msikiti ambao una kitu katika mapambo haya kukiwemo mnara mrefu ambao unakaribia kuyafikia mawingu kwa sababu ya urefu wake. Hii leo hakuna haja ya kitu hicho. Hapo kabla walikuwa wakisema kuwa hali ndio imepelekea kufanya hivo kwa sababu muadhini anapanda juu ya mnara ili sauti ya adhaana yake iweze kufika mbali iwezekanavyo. Hii leo adhaana inafika mara kumi kupitia kipaza sauti. Kutumia maelfu ya mapesa sio kwa ajili ya kuipamba misikiti kwa ndani peke yake bali kurefusha minara pia ni katika kufanyia israfu mali, sembuse kutaja ule uendaji kinyume wa Hadiyth zilizotangulia kutajwa juu ya kuipamba misikiti.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Hudaa wan-Nuur (1022)
  • Imechapishwa: 25/06/2020