Mgonjwa aliyeweza kulipa akazembea mpaka ameingiliwa na Ramadhaan nyingine

Swali: Sikufunga Ramadhaan kwa miaka miwili mfululizo kutokana na maradhi yaliyonipata. Ni kipi kinachonilazimu hivi sasa?

Jibu: Muda wa kuwa uliacha kufunga kutokana na udhuru unaokubalika katika Shari´ah ni lazima kulipa tu. Ni lazima kwako kulipa yale masiku uliyokula katika miaka miwili. Hakuna kitu juu yako ikiwa kuchelewesha kwako mpaka ukaingiliwa na Ramadhaan ya pili ni kutokana na udhuru unaokubalika kwa mujibu wa Shari´ah zaidi ya kulipa swawm yako. Lakini ikiwa kuchelewesha ni pasi na udhuru, bali ulichukulia wepesi, basi mbali na kulipa utatakiwa kumlisha masikini kwa kila siku iliyokupita. Hivo ndivo walivyojibu jopo la Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Lakini ikiwa ulilipa kabla ya kuingia Ramadhaan nyingine, basi utalazimika kulipa pasi na kulisha chakula. Lakini ukichelewesha kulipa mpaka kukaingia Ramadhaan nyingine, basi utatakiwa kulipa pamoja na kulisha chakula nusu pishi ya tende, ngano au mchele kwa kila siku pamoja na kutubia na kuomba msamaha.

Kuhusu ambaye ana udhuru hakuna kinachomlazimu pindi atapochelewesha kwa ajili ya maradhi. Katika hali hiyo hakuna kinachomlazimu mbali na kulipa. Kwa sababu Allaah anasema:

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safarini, hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Katika hali hiyo analazimika kulipa peke yake.

Lakini ambaye atachukulia wepesi na akaweza kulipa na asilipe mpaka ikafika Ramadhaan nyingine, basi huyu, mbali na kulipa, atapaswa kulisha masikini kwa kila siku moja iliyompita pamoja na kutubia.

[1] 02:184

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/10911/حكم-من-افطر-رمضان-في-عامين-لمرض
  • Imechapishwa: 24/03/2023