Mfano wa majina ya haramu na yaliyochukizwa

Ni jambo limependekezwa kuchagua jina zuri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika nyinyi [siku ya Qiyaamah] mtaitwa kwa majina yenu na majina ya baba zenu. Hivyo basi yafanyeni mazuri majina yenu.”[1]

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapenda majina mazuri na anaonelea kuwa ni haramu mtu kujinasibisha jina lake kuwa ni mja wa asiyekuwa Allaah. Kwa mfano mtu akaitwa ´Abdul-Ka´bah, Abdul-Masiyh, ´Abdul-´Aliy na ´Abdul-Husayn. Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“[Wanachuoni] wameafikiana juu ya uharamu wa kulinasibisha jina kwamba mtu ni mja wa asiyekuwa Allaah. Kwa mfano ´Abdul-´Umar, ´Abdul-Ka´bah na yanayofanana na hayo. Jina pekee lililobaguliwa ni ´Abdul-Muttwalib.”

´Abdul-Muttwalib ni kwa njia ya kutoa maelezo. Ni kama mfano wa Banuu ´Abdil-Daar na ´Abdush-Shams. Sio kwa njia ya kuunda utungaji wa jina hilo.

Ni jambo lenye kuchukiza kuitwa kwa jina lisilokuwa la sawa. Mfano wa majina hayo ni mtenda maasi (العاصي), mchungu (حنظلة), kitu kichungu (مرة) na huzuni (حزن). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amechukiza majina mabaya. Ni mamoja majina hayo ni ya watu au ni ya maeneo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika majina yenu yanayopendwa zaidi kwa Allaah ni ´Abdullaah na ´Abdur-Rahmaan.”[2]

Kwa hivyo mtu anapaswa kutilia umuhimu suala la kumchagulia mtoto wake mchanga jina zuri. Sambamba na hilo aepuke majina ya haramu na yaliyochukizwa. Kwa sababu kufanya hivo ni miongoni mwa haki za mtoto juu ya baba yake.

[1] Abu Daawuud.

[2] Muslim na wengineo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mulakhaswsw-ul-Fiqh (01/154-155)
  • Imechapishwa: 12/07/2020