Mawaidha ya walinganizi wote hawa yametoa faida gani?

Swali: Ni jambo linalojulikana ya kwamba ´Awwaam wengi hawasemi “Bismillaah” kabla ya kutawadha na wala hawajui kama kuna [wanachuoni] wanaoonelea kuwa kusema “Bismillaah” ni wajibu. Ni ipi hukumu ya wudhuu´ wao na swalah zao kutokana na Hadiyth iliyothibiti kuhusiana na wudhuu´?

Jibu: Ni lazima kwenu kuwafunza. Haya ni mapungufu yenu nyinyi [wanafunzi]. Lililo la wajibu ni nyinyi kuwafunza Ahkaam za wudhuu´. Miongoni mwazo ni kusema “Bismillaah” mwanzoni wa wudhuu´ halafu ndio mtu sasa atawadhe. Mtu akiacha Tasmiyah kwa kusahau hana juu yake kitu. Au ikiwa ameacha kwa ujinga hajui, huyu vilevile hana juu yake kitu. Ni wenye kupewa udhuru kwa kusahau na kwa ujinga. Lakini msiwaache watu juu ya ujinga wao.

Mimi naona watu wengi wenye kutoa mawaidha na kuwamkumbusha watu, kazi yao kubwa ni kutaka kuzitikisa nyoyo za watu, kuwapa mawaidha na kuwakumbusha lakini hawawafunzi watu. Hawawafunzi watu mambo kuhusiana na dini yao. Hili ni muhimu zaidi.

Lililo la wajibu kwa mlinganizi jambo la kwanza awafunze watu mambo kuhusiana na dini yao. Kuhusiana na mawaidha na kuwakumbusha, haya ni mambo yanayokuja baada ya kuwafunza mambo kuhusiana na Dini yao. Ama kuwatolea mawaidha na kuzitikisa nyonyo zao ilihali hawaijui dini yao, unawaacha juu ya ujinga wao, hili haliwanufaishi lolote.

Ni wajibu kwa walinganizi kutilia umuhimu jambo hili. Nalo ni kuwafunza watu mambo ya dini yao, twahara, swalah, zakaah, Hajj na ´Umrah, swawm na kadhalika. Wanachotakiwa ni kuwafunza, kuwahifadhisha, kuwafafanulia na kuwawekea wazi mambo haya.

Muhimu zaidi kuliko yote hayo wawafunze ´Aqiydah. Watu wengi wanatumbukia kwenye Shirki kubwa na ndogo pasina wao kujua. Wamewakuta watu wako katika haya na wakayarithi na hakukujitokeza yeyote akawawekea wazi. Wako wapi walinganizi wanaolingania katika dini ya Allaah? Hili ni tatizo kubwa. Ama nguvu zetu zote kuishia tu katika kutoa mawaidha na kuwakumbusha watu, hili haliwanufaishi lolote.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Buluugh al-Maraam (36) http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/blug–1431-08-15.mp3
  • Imechapishwa: 21/04/2015