Maswali kadhaa kuhusu ndoa na mitala

Swali: Je, kuna umri maalum kwa ajili ya ndoa kwa ajili ya mvulana au msichana? Je, kuna tofauti kati ya wanazuoni kuhusu suala la mitala?

Jibu: Ndoa haina umri maalum. Jambo linarejea pale mtu anapohitajia kuoa. Kijana wa kiume au wa kike akihitajia ndoa – wakati wowote – basi itakuwa ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwao wawili kuingia katika jambo hilo. Hakuna kikomo cha miaka. Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Enyi kongamano la barobaro! Yule atakayeweza miongoni mwenu kuoa basi na aoe. Hakika hilo linamfanya ainamishe macho na inahifadhi utupu wake.”

Swali: Lakini mara nyingi inakuwa baada ya kubaleghe?

Jibu: Mara nyingi inakuwa baada ya kubaleghe. Lakini ndapo mvulana ataona kabla ya kubaleghe au msichana akaozwa kabla ya kubaleghe hakuna ubaya wa kufanya hivo. Kuoa na kuolewa hakuna miaka maalum ambayo haifai kabla yake. Lakini baada ya kubaleghe haja inakuwa kubwa zaidi. Ndoa imewekwa katika Shari´ah wakati mtu anapoihitaji.

Kuhusu suala la mitala ni jambo waislamu wameafikiana juu ya kufaa kwake. Hakuna tofauti juu yake. Amesema (Ta´ala):

وَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تُقْسِطُوا فِي الْيَتَامَىٰ فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۖ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تَعْدِلُوا فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ

“Basi oeni waliokupendezeni katika wanawake wengine; wawili au watatu au wanne. Lakini mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu, basi [bakieni na] mmoja tu au ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki.”[1]

Suala la mitala wanazuoni wameafikiana kuhusu kufaa kwake. Lakini kwa sharti mtu ajue ndani ya nafsi yake kuwa ataweza kusimamia yale mahitaji ya wake zake ikiwa ni pamoja na matumizi, mavazi na malazi. Akiweza kusimamia yale uwezo wa kuwaruzuku basi aongeze mpaka wanawake wanne. Akiwa hawezi kufanya hivo na anachelea juu ya nafsi atadhulumu katika kugawa, matumizi na kutangamana na wale wake basi atosheke na mmoja:

فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تَعْدِلُوا فَوَاحِدَةً

“Lakini mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu, basi [bakieni na] mmoja tu.”

Makusudio ya uadilifu hapa ni katika kutangamana nao kwa wema, matumizi, mavazi, malazi na mengineyo katika mambo ambayo anaweza kuyafanyia uadilifu.

Kuhusu kumili kwa moyo na mapenzi ya moyo ni mambo ambayo mtu hawezi kuyashughulikia. Ndio maana amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَلَن تَسْتَطِيعُوا أَن تَعْدِلُوا بَيْنَ النِّسَاءِ وَلَوْ حَرَصْتُمْ ۖ فَلَا تَمِيلُوا كُلَّ الْمَيْلِ فَتَذَرُوهَا كَالْمُعَلَّقَةِ

“Wala hamtoweza kufanya uadilifu kati ya wake japokuwa mtatupia. Hivyo basi msimili muelemeo wote [kwa mke mmoja tu] mkamwacha mwengine kama ametundikwa.”[2]

Swali: Makusudio ya kumili ni kumili kwa moyo?

Jibu: Ndio. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akigawanya kati ya wake zake na akifanya uadilifu na akisema:

“Ee Allaah! Huu ndio mgawanyiko wangu katika yale ninayomiliki. Hivyo basi, usinilaumu katika yale nisiyomiliki.”

Bi maana kumili kwa moyo na mapenzi ya moyo.

Mtu hatoadhibiwa akiwapenda baadhi ya wakeze zaidi kuliko anavopenda wengine. Kwa sababu hiki ni kitu kilicho nje ya uwezo wake. Atachukuliwa hatua akidhulumu katika kugawanya na asifanye uadilifu. Haya ndio ambayo atachukuliwa hatua kwayo. Hapa ndipo pale ambapo haitofaa kwake kuoa wake wengi.

Swali: Idadi ya wanne haina tofauti kati ya wanazuoni?

Jibu: Idadi ni wanne. Hakuna tofauti kati ya wanazuoni. Hakuna anayesema chini ya hapo. Lakini yapo maoni ambayo ni dhaifu kabisa (شاذ) inayosema kuwa inafaa kuoa zaidi ya idadi hii. Hata hivyo haya ni maoni dhaifu kabisa. Maafikiano yanaonelea kinyume na hivo.

[1] 04:03

[2] 02:129

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (02/528-530)
  • Imechapishwa: 16/03/2022