Mama anataka mwongozo juu ya mwanae asiyeswali msikitini

Swali: Kuna mtu anakaribia miaka thelathini na mara nyingi anaswali nyumbani isipokuwa baadhi ya nyakati anahudhuria swalah za mkusanyiko na ijumaa. Lakini hakuonekani kwake upupiaji wa kulazimiana na swalah ya mkusanyiko. Mama yake anamg´ang´ania kulazimiana na swalah ya mkusanyiko. Wako ambao wamependekeza watu wamdhihirishie hasira na wasiketi naye pengine akarejea. Lakini mama yake anachelea juu yake na anasema kuwa anamsihi. Nataka mwongozo wa upambanuzi kuhusu mtu huyu juu ya dalili za ulazima wa swalah ya mkusanyiko na yanayompasa muislamu katika kumtii Allaah na kumshukuru juu ya zile neema alizomneemesha mtu kukiwemo uzima, ujana, afya njema na ukunjufu wa riziki. Ni ipi hukumu ya Shari´ah juu ya kuketi naye na kula naye akiwa na hali hii? Tunaomba na kutaraji ushauri mwingine utaompa mwongozo mama huyu na ni njia ipi anayotakiwa kutumia juu ya kijana huyu penigne akarejea.

Jibu: Hapana shaka yoyote kwamba kuswali mkusanyiko pamoja na waislamu wengine katika nyumba za Allaah ni miongoni mwa faradhi muhimu zaidi na ni katika nembo za Uislamu. Ni wajibu kwa kila ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia aipe umuhimu na aharakishe na kukimbilia kuswali katika mkusanyiko na waislamu wengine na ajiepushe kujifananisha na wanafiki. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Anayetaka kukutana na Allaah kesho hali ya kuwa muislamu basi azihifadhi swalah hizi pindi zinaponadiwa. Hakika Allaah amemuwekea Nabii Wake njia za uongofu – nazo ni njia za uongofu. Endapo mtaswali majumbani mwenu kama anavoswali nyumbani kwake huyu anayebaki nyuma basi mtakuwa mmeiacha njia ya Mtume wenu. Mkiacha njia ya Mtume wenu basi mtapotea. Tulikuwa tukiona hakuna anayeiacha – swalah ya mkusanyiko – isipokuwa ni mnafiki ambaye unatambulika unafiki wake au mgonjwa. Mtu – yaani katika Maswahabah – alikuwa kibebwa kati ya watu wawili – yaani mgonjwa au mtumzima mzee – mpaka anasimamishwa katika safu.”[1]

Bi maana kutokana na upupiaji wao mkubwa wa kuswali pamoja na mkusanyiko.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayesikia wito na asiutikie basi hana swalah isipokuwa kutokana na udhuru.”[2]

 Kukasemwa: “Ee Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu anhumaa)! Udhuru ni upi?” Akasema: “Khofu au maradhi.”

Imepokelewa katika “as-Swahiyh” kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema: “Bwana mmoja kipofu alisema: “Ee Mtume wa Allaah! Sina kiongozi wa kuniongoza msikitini. Je, ninayo ruhusa ya kuswali nyumbani kwangu?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza: “Je, wasikia wito wa swalah?” Akasema: “Ndio.” Akasema: “Basi imewajibika.”[3]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Sijakuonea wewe ruhusa.”[4]

Alitamani (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuzitia moto nyumba za wale wanaobaki nyuma. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Nimetamani niamrishe kuswaliwe ambapo ikasimamishwa kisha nikamwamrisha mtu awaswalishe watu halafu nikaondoka na kikosi cha wanamme walio na vifurushi vya kuni kuwaendea watu ambao hawashuhudii swalah nikazichoma nyumba zao kwa moto.”[5]

Namna hii ndivo anavosema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika upokezi wa Imaam Ahmad:

“Isingelikuwa wanawake na watoto waliyomo katika majumba basi ningezichoma moto.”[6]

Tunachokusudia ni kwamba kuswali mkusanyiko ndani ya nyumba za Allaah – ambayo ni ile misikiti – ni jambo la faradhi na la lazima. Ni alama ya waislamu na alama za watu wa haki. Kubaki nyuma na badala yake kuswali majumbani ni alama ya wanafiki. Kwa hiyo haitakikani kwa muislamu kujifananisha na wanafiki ambao Allaah (Subhaanah) amesema juu yao:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا مُّذَبْذَبِينَ بَيْنَ ذَٰلِكَ لَا إِلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ وَلَا إِلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ

“Hakika wanafiki wanafikiri wanamhadaa Allaah na hali Yeye ndiye Mwenye kuwahadaa na wanaposimama kuswali basi husimama kwa uvivu, wakijionyesha kwa watu na wala hawamtaji Allaah isipokuwa kidogo tu. Wenye kuyumbayumba kati ya hayo, huku hawako wala huko hawako.”[7]

Ametaja (Subhaanah) sifa tano za wanafiki:

1 – Wanafikiri wanamdanganya Allaah na waumini. Hawana nasaha wala amana. Bali walichonacho ni vitimbi, udanganyifu na kuwafanya njama dhidi ya waislamu katika kutangamana nao.

2 – Wanaposimama kwa ajili ya kuswali husimama kwa uvivu. Kwa maana nyingine hawana uchangamfu kwa kutokuwa na imani. Inahusiana na kujionyesha tu.

3 – Hawamtaji Allaah isipokuwa kidogo tu. Wanamtaja Allaah kidogo, jambo ambalo kunatambulika kwao ughafilikaji.

4 – Ni wenye kujionyesha kwa watu kwa matendo yao. Hawana jambo la kumtakasia Allaah nia. Walicholenga kwa matendo yao ni kujionyesha, watu wawasikie na kutafuta masifa. Hawana jambo la kumtakasia Allaah nia.

5 – Ni wenye kuyumbayumba na hawana uimara wala lengo lililonyooka. Bali mara wanakuwa pamoja na waumini na mara wanakuwa pamoja na makafiri. Hawana kanuni, dini imara wala imani ya kweli. Bali waumini wakishinda na wakapata nusura basi wanakuwa pamoja na waumini. Makafiri wakishinda wanakuwa pamoja na makafiri. Hii ndio hali ya wanafiki. Ni vipi basi muumini ataridhia kujifananisha nao katika kujiweka nyuma na kuacha kuswali katika mkusanyiko?

Mama ambaye amemnasihi mwanae kuswali pamoja na mkusanyiko amefanya vyema. Hili ndio jambo la lazima kwake. Ni lazima kwake vilevile kuendelea katika jambo hilo, amnasihi siku zote na amkate akikataa na asitekeleze. Aidha atake msaada kwa Allaah kisha wale jamaa anaowaona kama mfano wa baba yake, kaka yake mkubwa, ami yake na wengineo akiwa yuko na jamaa wema basi amtake msaada Allaah kisha wao.

Kwa kumalizia ni kwamba yule anayetambulika kukosa mkusanyiko anastahiki kukatwa na kutiwa adabu na mtawala mpaka anyooke na kuchunga swalah ya mkusanyiko.

Kama inavotambulika kuacha kuswali katika mkusanyiko ni miongoni mwa sababu kubwa zinazopelekea kuiacha kabisa. Ugonjwa huyu uliyomfanya kubaki nyuma utampelekea mara nyingi kuiacha na kutoipa umuhimu; mara atakuwa mwenye kuswali na mara atakuwa si mwenye kuswali. Hili litampelekea kujionyesha; akiwaona wale anaowastahi, ataswali, na akipwekeka, ataacha. Hii ndio hali ya wanafiki. Kwa hiyo ni lazima kutahadhari.

Ni lazima kwa mama, jamaa zake wanamme huyo na marafiki zake kumshauri na wamsaidie mama yake dhidi yake. Wamkate akiendelea juu ya batili na kubaki kwake nyuma.

[1] Muslim (1046).

[2] Ibn Maajah (793).

[3] Muslim (653) na an-Nasaa´iy (850).

[4] Abu Daawuud (552) na Ibn Maajah (792).

[5] Ahmad (9202), al-Bukhaariy (7224) na Muslim (651).

[6] Ahmad (8578).

[7] 04:142-143

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/24-27)
  • Imechapishwa: 19/10/2021