15. Ni nini maana ya kuamini siku ya Mwisho na imejumuisha nini?

´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 15: Ni nini maana ya kuamini siku ya Mwisho na imejumuisha nini?

Jibu: Kila kilichotajwa katika Qur-aan na Sunnah katika mambo yatayopitika baada ya mauti. Yote haya yanaingia katika imani ya kuamini siku ya Mwisho.

Mfano wa hilo ni kama hali za ndani ya makaburi kama neema na adhabu zinazopatikana ndani yake.

Mfano wa hilo ni kama hali za siku ya Qiyaamah kama hesabu, thawabu, adhabu, kugawiwa madaftari, mizani na uombezi.

Mfano wa hilo ni Pepo na Moto, sifa zake, sifa za wakazi wake na yale yote Allaah aliyowaandalia [wakazi wake]. Yote hayo yanaingia katika imani ya kuamini siku ya Mwisho.

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amebainisha imani ya kuamini siku ya mwisho kwa kusema:

“Kila kilichotajwa katika Qur-aan na Sunnah katika mambo yatayopitika baada ya mauti. Yote haya yanaingia katika imani ya kuamini siku ya Mwisho.”

Maneno yake mtunzi wa kitabu:

“Mfano wa hilo ni kama hali za ndani ya makaburi… “

Hali za ndani ya kaburi ni kama kumwamini Munkar na Nakiyr, maswali yao pamoja na jawabu la mja mwema muumini na muovu mtenda dhambi pamoja na yale yanayopelekea kwa kila kimoja katika hivyo viwili katika neema juu ya mwema na adhabu juu ya kafiri muovu kama ilivyotajwa katika Qur-aan na Sunnah.

Maneno yake mtunzi wa kitabu:

“… kama neema na adhabu zinazopatikana ndani yake.”

Kaburi ni kituo kinachopambanua kati ya maisha ya kidunia na maisha ya Aakhirah. Huko kila mja atakutana na kile alichotumikia. Manabii na Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) hali zao ndani ya kaburi sio kama hali za watu wengine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa alikutana na baadhi ya Mitume wakati wa safari yake ya kwenda juu mbinguni juu ya ngazi zao katika mawingu[1].

Mfano mwingine ni ile ndoto ambayo imepokelewa na al-Bukhaariy kupitia kwa Samurah bin Jundub (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) amesema kwamba ameota kuhusu adhabu za watenda madhambi; mtu mwenye kulala na kupitwa na swalah ambapo kichwa chake kilikuwa kinavunjwa kwa jiwe, mwenye kuzungumza akasema uongo na uongo ule ukaenea kwenye midomo ya watu ambapo anaadhibiwa kwa kuingizwa ndoano kwenye mdomo mmoja kisha inavutwa kwenye mdomo mwingine kwa nyuma yake, wanawake wazinzi na wanamme wako mahala penye moto kama mfano wa oveni, mlaji ribaa anaogelea kwenye mto wa damu na kwamba alimpitia Ibraahiym kipenzi wa hali ya juu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamkuta yuko pamoja naye watoto wa waislamu wanaokufa kabla ya kubaleghe[2].

Maneno ya mtunzi wa kitabu:

“Mfano wa hilo ni kama hali za siku ya Qiyaamah kama hesabu, thawabu, adhabu, kugawiwa madaftari, mizani na uombezi.”

Miongoni mwa hayo ni kutetemeka kwa ardhi:

إِذَا زُلْزِلَتِ الْأَرْضُ زِلْزَالَهَا

“Ardhi itakapotetemeshwa kwa mtetemeko wake!”[3]

bahari kushika moto:

وَإِذَا الْبِحَارُ سُجِّرَتْ

“… na bahari zitapowashwa moto.”[4]

majibali kusambuka na kuwa udongo:

وَبُسَّتِ الْجِبَالُ بَسًّا

“… na itapondwapondwa milima.”[5]

ardhi ambapo inageuka na kuwa ardhi nyingine:

يَوْمَ تُبَدَّلُ الْأَرْضُ غَيْرَ الْأَرْضِ وَالسَّمَاوَاتُ

“… na Siku ardhi itakapobadilishwa kuwa ardhi nyingine na mbingu pia.”[6]

kukunjwa kwa ardhi na mbingu:

وَالسَّماوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ

“Mbingu zote zitakamatwa mkononi Mwake wa kuume siku ya Qiyaamah.”[7]

Allaah ambapo atasema:

“Mimi ndiye Mfalme! Wako wapi wenye jeuri? Wako wapi wenye kiburi?” Kisha atazikunja ardhi saba, kisha atazishika kwa mkono Wake wa kushoto kisha atasema: “Mimi ndiye Mfalme! Wako wapi wenye jeuri? Wako wapi wenye kiburi?”[8],

na Israafiyl atapuliza mara ya kwanza parapanda kuwashtua waliohai, kisha atapuliza mara ya pili afe kila aliyehai na atapuliza mara ya tatu kuwafufua waliyomo ndani ya makaburi.

Yote haya ni katika hali zinazojitokeza kabla ya Qiyaamah. Kisha baada ya hapo watasimama watu kutoka ndani ya makaburi yao na wakusanyike mbele ya Mola wao. Watamsikia mwenye kuita na watamfuata:

فَتَوَلَّ عَنْهُمْ ۘ يَوْمَ يَدْعُ الدَّاعِ إِلَىٰ شَيْءٍ نُّكُرٍ خُشَّعًا أَبْصَارُهُمْ يَخْرُجُونَ مِنَ الْأَجْدَاثِ كَأَنَّهُمْ جَرَادٌ مُّنتَشِرٌ مُّهْطِعِينَ إِلَى الدَّاعِ ۖ يَقُولُ الْكَافِرُونَ هَـٰذَا يَوْمٌ عَسِرٌ

“Basi jitenge nao mbali. Siku atakayoita mwitaji kuliendea jambo baya mno la kuogofya. Macho yao yakiwa dhalili, watatoka kwenye makaburi kama kwamba wao ni nzige waliosambaa. Wenye kukimbia mbio huku wakibenua shingo zao wakielekea kwa mwitaji, makafiri watasema: “Hii ni siku ngumu!”[9]

Hapo watasimama kisimamo kirefu kabisa. Jua litasogezwa karibu na vichwa vyao. Jasho zao zitawafunika kiasi cha kwamba baadhi jasho litawafika puani. Baada ya kisimamo cha muda mrefu waumini watamwendea Aadam, kisha Nuuh, kisha Ibraahiym, kisha Muusa na kisha ´Iysaa wawatake kuwafanyia uombezi wa kufanyiwa hukumu. Watapofika kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atasema:

“Mimi ndiye mstahiki.”[10]

Baada ya hapo kutafuatia hesabu na yatagawanywa madaftari. Kila mmoja atakadhibiwa daftari lake, baadhi watapewa kwa mkono wa kuume, wengine kwa mkono wa kushoto nyuma ya mgongo. Matendo yatapimwa. Waumini watapewa nuru, wakiwemo wanafiki, kisha baadaye itazimwa nuru ya wanafiki. Hii ndio adhabu yao ya kwanza huko Aakhirah. Waumini wataokolewa. Hii ndio thawabu yao ya kwanza huko Aakhirah. Waumini watapita juu ya njia ilionyooka na makafiri watavutwa kuelekea Motoni. Amesema (Ta´ala):

وَيَوْمَ يُحْشَرُ أَعْدَاءُ اللَّـهِ إِلَى النَّارِ فَهُمْ يُوزَعُونَ

“Siku watakayokusanywa maadui wa Allaah kwenye moto, nao wakigawanywa kwa makundi.”[11]

Baada ya hapo kutafanyika maombezi. Waumini watalipwa thawabu Peponi na yale yote yanayohusiana na hayo, na makafiri wataadhibiwa Motoni na yale yote yanayohusiana na hayo.

[1] al-Bukhaariy (3887) na Muslim (162).

[2] al-Bukhaariy (7047).

[3] 99:1

[4] 56:5

[5] 56:5

[6] 14:48

[7] 54:6-8

[8] Muslim (2788).

[9] 54:6-8

[10] al-Bukhaariy (7510) na Muslim (193).

[11] 41:19

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 84-89
  • Imechapishwa: 19/10/2021