Malengo ni sisi tufanye matendo, na sio kufahamu peke yake

Tunakabiliwa na msimu mtukufu ambao ni zile siku kumi za mwanzo za Dhul-Hijjah ambazo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Hakuna masiku ambayo matendo mema yanapendwa zaidi na Allaah ndani yake kama  masiku haya kumi.”

Bi maana matendo mema katika siku kumi za mwanzo za Dhul-Hijjah yanapendeza zaidi kwa Allaah kuliko matendo mema katika siku kumi za mwisho za Ramadhaan. Kwa sababu Hadiyth ni yenye kuenea na kukata kabisa kwamba hakuna masiku ambayo  matendo mema yanapendeza zaidi kwa Allaah kuliko masiku haya.

Aliyesema maneno haya ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ndiye kiumbe mjuzi zaidi juu ya Shari´ah ya Allaah, juu ya Allaah na mjuzi zaidi wa yale anayoyapenda Allaah.

Kwa hiyo usishangazwe ukimsikia ambaye anasema kuwa matendo mema katika siku kumi za Dhul-Hijjah ni bora kuliko matendo mema katika masiku kumi ya Ramadhaan. Usishangazwe ukisikia hivo. Kwa sababu jambo hili liko na dalili kutoka katika maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Maneno haya yaliyosemwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) makusudio yake si kwamba tufahamu peke yake kwamba matendo mema katika masiku haya kumi yanapendeza zaidi kwa Allaah kuliko masiku mengine. Malengo yake ametaka tufahamu na tufanye matendo. Watu wanatakiwa kufanya matendo mema kwa wingi katika masiku kumi ya mwanzo katika Dhul-Hijjah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binothaimeen.net/content/17549
  • Imechapishwa: 24/07/2020