Makemeo makali kwa anayeacha swalah za mkusanyiko msikitini na swalah ya ijumaa

Swali: Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliulizwa juu ya mtu ambaye anasimama usiku kuswali na anafunga mchana lakini hata hivyo hashuhudii swalah ya ijumaa wala swalah za mkusanyiko ambapo akasema kuwa yuko Motoni. Ni upi usahihi wa Hadiyth hii tukufu?

Jibu: Athar hii ni yenye kutambulika kutoka kwa Ibn ´Abbaas na imesihi kupokelewa kutoka kwake (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Inafahamisha kwamba kuacha swalah ya ijumaa na swalah za mkusanyiko ni miongoni mwa sababu za kuingia Motoni . Imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Wakome watu kuacha [swalah za] ijumaa au atazipiga muhuri nyoyo zao kisha watakuwa miongoni mwa waghafilikaji.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah na Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhum). Abu Daawuud amepokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Mwenye kuacha [swalah za] ijumaa tatu basi Allaah atapiga muhuri kwenye moyo wake.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kusikia adhaana na asiitikie basi hana swalah isipokuwa akiwa na udhuru.”

Kwa hiyo ni lazima kwa muislamu kufanya haraka kuitikia wito wa ijumaa na wa swalah ya mkusanyiko na asiache kufanya hivo. Pale atapoacha kufanya hivo bila udhuru unaokubalika katika Shari´ah – kama mfano wa ugonjwa na khofu basi ni mwenye kutishiwa Moto ingawa atakuwa ni mwenye kufunga mchana na kusimama usiku.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/252)
  • Imechapishwa: 11/09/2021