65. Madhara yanayopelekea katika ´Aqiydah ya Qadariyyah na Jabriyyah

5 – Kuhusu mambo yanayopelekea katika ´Aqiydah ya Jabriyyah na Qadariyyah. Inapelekea katika mambo ya khatari yafuatayo:

1 – ´Aqiydah ya Qadariyyah inapelekea katika kuthibitisha waungu wengi pamoja na Allaah. Hii ni shirki katika matendo ya Allaah. Kwa ajili hii ndio maana wameitwa kuwa ni ´waabudu moto wa Ummah huu`.

2 – ´Aqiydah ya Jabriyyah inapelekea kumsifu Allaah kwa dhuluma na kwamba anawaadhibu waja kwa kitu ambacho hawakufanya wao, bali kimefanya Allaah. Allaah anawaadhibu kwa kitu ambacho wao hawakufanya. Wao wanaendeshwa tu pasi na khiyari wala kutaka kwao. Huku ni kumsifu Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa dhuluma ya kwamba anawaadhibu waja kwa kitu ambacho hawakufanya wao bali kimefanya Yeye Mwenyewe. Uharibifu wa madhehebu haya batili haujifichi. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

“Na wala hamtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyatenda.” (36:54)

Amefungamanisha adhabu kwa kufuru, maasi na madhambi kama ambavyo vilevile amefungamanisha utiifu kwa mambo ya utiifu na ya kheri. Allaah hamdhulumu yeyote:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا

“Hakika Allaah hadhulumu [kiumbe yeyote] uzito wa atomu na ikiwa ni [tendo] jema huizidisha.” (04:40)

Huu ndio uadilifu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Miongoni mwa uadilifu Wake ni kuwa hayaongezi madhambi. Analipa kwa mfano wake. Katika fadhilah Zake ni kuwa analiongeza jema moja kwa kupenda Kwake Mwenyewe (Subhaanahu wa Ta´ala).

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا

“Hakika Allaah hadhulumu [kiumbe yeyote] uzito wa atomu na ikiwa ni [tendo] jema huizidisha.”

Huku kuongezewa ni fadhilah kutoka kwa Allaah mpaka kufikia kumi mfano wake mpaka kufikia mia saba na zaidi ya hivyo. Kuhusu maovu Allaah analipa mfano wake na hazidishi juu yake. Haya ni kutokana na uadilifu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Lakini Jabriyyah wanamsifu Allaah kwa dhuluma ya kwamba anawaadhibu waja kwa matendo Aliyofanya Mwenyewe. Wanasema kuwa wao hawakufanya kitu wanapelekwa kama chombo na kama upepo hewani. Hii ni ´Aqiydah batili.

3 – ´Aqiydah zao zinapelekea kuacha kufanya sababu na mtu akasema kuwa midhali Ameshakadiria na kupanga basi mimi nakaa na nilichokadiriwa kitanijia.

4 – ´Aqiydah ya Mu´tazilah, kama tulivyotangulia kusema, inapelekea katika kushirikisha katika matendo ya Allaah.

5 – ´Aqiydah yao inapelekea katika madhara makubwa, ambayo ni kumfanya Allaah (´Azza wa Jall) kutoweza na kwamba kunapitika katika ufalme Wake kile asichokitaka na kukipenda. Huku ni kumsifu Allaah (´Azza wa Jall) kutokuwa na uwezo. Hii ni khatari kubwa.

´Aqiydah zote mawili ni batilifu na zinapelekea katika madhara makubwa. Kuhusu ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah iko kati kwa kati na adilifu katika mambo yote.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 151-153
  • Imechapishwa: 12/01/2024