Madhambi aliyofanya yanamfanya kuwa na wasiwasi

Swali: Kuna mtu amechupa mpaka katika nafsi yake hata hivyo ametubia kwa Mola Wake. Licha ya hivyo anaogopa kutokana na dhambi zilizotangulia, kitu ambacho kimesababisha kuwa na khofu ambayo imepelekea katika wasiwasi. Tunaomba mwongozo ili aondokane na wasiwasi hii?

Jibu: Mtu akichupa mpaka juu ya nafsi yake kisha Allaah akamwongoza na akamtunuku tawbah amshukuru Allaah. Atambue kuwa Allaah amemtunuku tawbah kwa ajili ya rehema na fadhilah Zake juu yake (Subhaanah). Lengo ni kutaka kumsafisha kutokamana na maasi. Apate bishara njema na ajichunge kutokana na shaytwaan na ushawishi wake. Shaytwaan anaweza kumtumbukiza ndani ya wasiwasi na kuwa na dhana mbaya. Kwa hivyo atahadhari na jambo hilo na wala asimtii adui wa Allaah. Kwani hakika Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameeleza kwamba mja anapotubu, akaamini na akatenda matendo mema, basi Allaah humsamehe na humbadilishia maovu yake yakawa mema. Amesema (Subhaanah):

وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ

“Hakika Mimi ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema kisha akanyooka barabara.” (20:82)

Vilevile imekuja katika Hadiyth Swahiyh isemayo:

“Yeyote anayetubia kutokana na dhambi ni kama ambaye hana dhambi.”

Kwa hivyo anayetubia Allaah anamsamehe maovu yake na kumfutia makosa yake. Kwa hivyo ni lazima kwako, ee ndugu, kutubu na kulazimiana nayo. Sambamba na hilo tahadhari na wasiwasi na dhana uvo ambazo Allaah amekuharamishia.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3699/بم-ينصح-من-تاب-ويخاف-الذنوب-السابقة
  • Imechapishwa: 06/06/2022