Swali: Baadhi ya ndugu zetu Pakistan ambao wanajuzishia baadhi ya makundi yao kuingia katika bunge la kipakistan wanasema kuwa inatofautiana kiasi kikubwa na mabunge nchi nyinginezo. Ingawa Shari´ah imeorodheshwa kama chaguo na wengi wanapata kura zao katika nchi nyingine, hali ni tofauti kabisa na ilivyo Pakistan. Wanachokusudia ni kwamba kushiriki kwao katika bunge kunawafanya kuwa na nguvu na kufanya Shari´ah itume huko. Unasemaje juu ya hilo?

Jibu: Mimi naona kama wanavoona wanazuoni wengine kwamba kilichojengeka juu ya kitu kibovu nacho kinakuwa kibovu. Ninachojua ni kwamba kanuni zote za kibunge hazikujengeka juu ya Shari´ah ya kiislamu. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ

“Na jambo lao hushauriana baina yao.”[1]

Wanazuoni wanasema kuwa maandiko yote yaliyokuja kwa njia ya ujumla, yaliyoachiwa na yaliyoenea ndani ya Qur-aan yamebainishwa katika Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambazo wanazuoni wamezigawanya katika sampuli tatu:

1 – Kimaneno.

2 – Kivitendo.

3 – Kuyakubali.

Katika sampuli ya kukubali naweza kuongeza Sunnah ya kuacha, pengine isitajwe katika vitabu vya wanazuoni vinavyotambulika. Tunajua kuwa yale aliyoyaacha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Sunnah kwetu pia ni sisi kuyaacha, jambo ambalo limepambanuliwa na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika vitabu vyake vilivyojaa elimu iliokomaa. Kile ninachotaka kufikia ni kama maneno Yake Allaah (´Azza wa Jall):

وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ

“Na jambo lao hushauriana baina yao.”

yanahusu waislamu wote. Wanamaanisha wema na waovu? Wanamaanisha wanazuoni na wajinga? Hapana shaka yoyote kwamba jawabu litakuwa hapana. Vipi basi tutaifahamu Aayah hii na mfano wake?

وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ

”Na washauri katika mambo.”[2]

Nimesema mwanzoni mwa jibu kwamba andiko linaweza kuwa la kijumla, lililoachiwa au lililoenea na hivyo baadaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akalibainisha. Aayah isemayo:

وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ

“Na jambo lao hushauriana baina yao.”

limeachiwa. Aayah inayosema:

وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ

”Na washauri katika mambo.”

ni amri ilioenea. Ni vipi kuyafanyia kazi yote mawili? Hatuna shaka yoyote kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hawashauri Maswahabah wote. Alikuwa akiwashauri kikosi cha Maswahabah kadhaa walio bora. Nasema kuwa kilichojengeka juu ya kitu kibovu nacho kinakuwa kibovu.

Je, bunge hili la kipakistan linatofautiana na mabunge mengine yaliyochanganya waislamu na makafiri? Nilikuwa nataraji kuwa liko na waislamu peke yao, lakini haikuchukua muda mrefu ikaja kuonyesha kuwa liko na waislamu na makafiri. Tunasikitika kwa hilo. Tunasikitika vilevile wanaposema kuwa linatofautiana na mabunge mengine. Sisemi kuwa halitofautiani kwa kuzingatia kuwa bunge la kifaransa linaweza kutofautiana na bunge la kingereza, bunge la kingereza na bunge la kimarekani na kadhalika. Kilicho muhimu kwetu ni kwa njia gani bunge hili la kipakistan linatofautiana na mabunge mengine ya kiislamu.

Je, wanashiriki humo waislamu wema na waovu? Bila shaka. Ikiwa wapo makafiri katika mabunge yao basi kwa asimilia kubwa wapo pia waislamu watenda madhambi.

Je, ni wanazuoni peke yao ndio wanagombea au anagombea kila awezaye? Anagombea kila awezaye. Kwa msemo mwingine yamebainika yaliyomo ndani katika kichwa cha khabari. Bunge hili halina tofauti kwa njia ya kimuundo. Nimesema punde kwamba katiba za makafiri zinaweza kutofautiana zenyewe kwa zenyewe. Kinachotuhusu sisi ni kuwepo bunge katika nchi ya kiislamu ambalo baadhi wanadai kuwa linatofautiana na mabunge mengine.

Bunge hili ambalo liko na majanga yote haya linatofautiana na mabunge mengine ikiwa raisi anataka kulitengua bunge au kulisimamisha kwa kipindi fulani?

Muulizaji: Hapana.

al-Albaaniy: Kuna faida gani basi ya bunge kama hili?

Nawanasihi ndugu zetu walazimiane na misikiti yao, masomo yao na duara zao za kielimu kwa mujibu wa Salafiyyah na si mujibu wa Suufiyyah. Hili ni bora kwao.

[1] 42:38

[2] 03:159

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Hudaa wan-Nuur (930) Tarehe: 1417-04-09/1996-08-24
  • Imechapishwa: 10/08/2022