07. Msongamano kwa ajili ya kuswali maeneo pa Ismaa´iyl

Swali 07: Tunawaona baadhi ya watu wanasongamana kwa ajili ya kuswali maeneo pa Ismaa´iyl (حجر إسماعيل). Ni ipi hukumu ya kuswali ndani yake? Je, ni jambo lina sifa ya kipekee?

Jibu: Kuswali katika maeneo pa Ismaa´iyl ni jambo linapendeza. Kwa sababu ni sehemu ya Ka´bah. Imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kwamba aliingia ndani ya Ka´bah mwaka wa Ufunguzi na akaswali ndani yake Rak´ah mbili.”

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kutoka kwa Bilaal (Radhiya Allaahu ´anh). Imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa alisema kumwambia ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) pindi alipotaka kuingia ndani ya Ka´bah:

“Swali maeneo [pa Ismaa´iyl]. Kwani hakika ni sehemu ya Nyumba.”

Kuhusu swalah za faradhi tahadhari zaidi ni kutoziswali ndani ya Ka´bah au katika maeneo [pa Ismaa´iyl]. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakufanya hivo. Isitoshe baadhi ya wanazuoni wamesema kuwa haisihi ndani ya Ka´bah wala katika maeneo [pa Ismaa´iyl] kwa sababu ni sehemu katika Ka´bah.

Kutokana na hayo inapata kufahamika kwamba kilichosuniwa ni kuswali swalah za faradhi nje ya Ka´bah na nje ya maeneo pa Ismaa´iyl kwa ajili ya kumuigiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwa ajili ya kutoka nje ya tofauti za wanazuoni wanaosema kuwa haisihi ndani ya Ka´bah wala katika maeneo pa Ismaa´iyl.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 07-08
  • Imechapishwa: 10/08/2022