Enyi watu! Hakika mwezi wa Ramadhaan uko njiani kusema kwaheri na kuondoka kwake kunakaribia. Utamshuhudilia yule ambaye alifanya vizuri miongoni mwa wale waliotenda mema na pia utashuhudilia dhidi ya yule ambaye alifanya vibaya miongoni mwa wale waliokwenda kinyume na kuasi. Ee nyinyi mlio na mioyo na akili! Iko wapi nuru ya kujichunga na kukubali gizani? Ziko wapi dalili za miili na ngozi zinazojulisha juu ya ukweli na kujitahidi katika mwezi wa Ramadhaan? Hapana shaka kwamba uko njiani unaondoka, upatilizeni na burudikeni na zile siku zake zilizobaki na msizipoteze. Huenda Ramadhaan isizibwe pengo lake na mwezi mwingine. Katika mwezi huu nyoyo zinaimarishwa, madhambi yanasamehewa na kupewa amani kila yule ambaye ni mwoga. Misikiti imejaa. Michana yake kunatolewa swadaqah na swawm, nyusiku zake ni kisomo na kusimama kuswali. Siku zake zote ni zenye salama. Malaika wanashuka chini. Wafungwa huachiliwa huru. Hivyo basi kimbilieni kutumia fursa, kwa sababu pengine wengi wenu hamtoudiriki tena mwezi huu mwaka ujao. Yule aliye na furaha na akafaulu amepata faida. Yule aliyepitwa na ngawira na thawabu zote amekula hasara. Amkeni kutoka usingizini na jiandaeni kwa ajili ya siku ya Qiyaamah. Kithirisheni matendo yenu kwa ajili ya siku ya mavuno.

Enyi waja wa Allaah! Kuondoka kwa mwezi huu kumekaribia. Pengine haitowezekana kupata tena fursa kama hii. Laiti ningejua ni nani ambaye amekula hasara kwa sababu ya udanganyifu na ni nani aliyetekeleza ahadi ya Mwingi wa huruma. Ee mzembeaji! Tumia fursa ya kumtii Mwingi wa kutoa na yakimbilie mambo ya kheri. Je, hivi kuna malipo ya wema kama si wema mfano wake? Ee mghafilikaji! Amka na tazama zile siku zilizobaki zilizombele yako na chunga Ramadhaan isije kushuhudia dhidi yako kutokana na ubaya wa dhambi zako. Jiandae kuondoka kwako kabla hujachelewa. Allaah amrehemu yule ambaye anatubu mbele ya Mola Wake ukweli wa kutubia. Aliyefuzu kikweli ni yule aliyerejea Kwake, akatengeneza kwa siku hizi zilizobaki yale yote aliyozembea hapo kabla na akajipinda mpaka mwisho. Matendo yanazingatiwa ule mwisho wake.

  • Mhusika: Imaam Swiddiyq Hasan Khaan al-Qanuujiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Maw´idhwah al-Hasanah, uk. 108-109
  • Imechapishwa: 21/05/2020