Kwa uchaji Allaah humzidishia mtu fahamu na firasa

Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَتَّقُوا اللَّـهَ يَجْعَل لَّكُمْ فُرْقَانًا وَيُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۗوَاللَّـهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ

“Enyi mlioamini! Mkimcha Allaah atakupeni Kipambanuzi na atakufutieni maovu yenuna akusameheni; na Allaah ni Mwenye fadhilah kuu.” (08:29)

Haina shaka ya kwamba kila ambavyo elimu ya mtu inazidi basi maarifa na upambanuzi wake wa haki na batili, mambo ya madhara na yenye manufaa huzidi. Katika hili kunaingia pia uelewa ambao Allaah anamfunulia mja.

Hakika kumcha Allaah ni sababu ya fahamu kubwa na nguvu. Fahamu ikiwa na nguvu basi elimu huzidi. Utaona watu wawili wote wamehifadhi Aayah katika Qur-aan. Mmoja wao katika Aayah hiyo anatoa kwa mfano hukumu tatu. Mwingine anatoa hukumu nne, tano, kumi au zaidi kwa kiasi na fahamu ambayo Allaah atakuwa amemjaalia. Kwa hivyo kumcha Allaah ni sababu ya fahamu kuzidi.

Vilevile kunaingia firasa (الفراسة). Allaah humjaalia mtu mwenye kumcha firasa ya kuweza kupambanua kati ya watu. Pale anapomtazama mtu tu basi anajua kuwa ni msema kweli au mwongo, mwema au mwovu. Pengine akaweza hata kumhukumu mtu kabla ya kumuashiria au kujua kitu kuhusu yeye. Hili linatokamana na firasa ambayo Allaah amemtunukia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/519)