Kuweka wakati wa kujizuia (Imsaak) kabla ya kuchomoza Fajr ni Bid´ah na kuvuka mipaka

Swali 429: Tunaona baadhi ya kalenda za mwezi wa Ramadhaan wanaweka kitu kinachoitwa “wakati wa kujizuia” (الإمساك) na wanaweka takriban dakika kumi au robo saa kabla ya kuingia swalah ya Fajr. Je, kitendo hichi ni katika Sunnah au ni katika Bid´ah?

Jibu: Hii ni katika Bid´ah. Ni jambo halina msingi katika Sunnah. Bali Sunnah inaonyesha kinyume na hivo. Kwa sababu Allaah amesema katika Kitabu Chake kitukufu:

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe wa alfajiri kutokana na uzi mweusi.” (02:187)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Bilaal anaadhini usiku. Hivyo kuleni na kunyweni mpaka msikie adhaana ya Ibn Umm Maktuum. Kwani yeye haadhini mpaka kuchomoze alfajiri.”[1]

Kujizuia huku ambako kunafanywa na watu ni nyongeza juu ya yale aliyoyafaradhisha Allaah (´Azza wa Jall). Hivyo ni batili. Hakika kitendo hicho ni katika kuchupa mipaka katika dini ya Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wameangamia wenye kuchupa mipaka! Wameangamia wenye kuchupa mipaka! Wameangamia wenye kuchupa mipaka!”[2]

[1] al-Bukhaariy (1918) na Muslim (1092).

[2] Muslim (2670).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Arkaan-il-Islaam, uk. 481
  • Imechapishwa: 14/05/2019