Haijuzu kuwaombea du´aa mbaya. Kuwaombea du´aa mbaya ni uasi wa kimaana, kama kuwafanyia uasi kwa silaha. Yule ambaye ameomba dhidi yao ni kwa sababu haoni kuwa wana utawala juu yake. Ni lazima kuwaombea uongofu na kutengemaa, na si kuomba dhidi yao.

Huu ni msingi miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Ukimuona mtu anamuombea mtawala du´aa mbaya, basi utambue kuwa amepotea katika ´Aqiydah yake na hafuati mfumo wa Salaf. Baadhi ya watu wanaweza kufanya hivo kutokana na ghera na kukasirika kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall), lakini ghera na hasira hiyo imewekwa mahali ambapo si pake na inaishilia kuleta majanga. Imaam al-Fudhwayl bin ´Iyaadh (Rahimahu Allaah) amesema:

“Lau ningejua kuwa nina du´aa moja yenye kukubaliwa, basi ningemwombea nayo mtawala.”[1]

Yamepokelewa maneno kama hayo kutoka kwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah). Imaam Ahmad alifanya subira wakati wa mtihani. Haikuthibiti kutoka kwake ya kwamba aliwaombea watawala wake du´aa mbaya au aliwazungumza vibaya. Bali alifanya subira. Mwisho mzuri ulikuwa kwake. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Wale wanaowaombea du´aa mbaya watawala wa waislamu hawafuati ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Vivyo hivyo kuhusu wale wasiowaombea du´aa nzuri. Hiyo ni alama inayojulisha kuwa wanaenda kombo na ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

[1] Abu Nu´aym (8/91) na al-Khallaal (9).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujj al-Qawiyyah ´alaa Wujuub-id-Difaa´ ´an-id-Dawlah as-Su´uudiyyah, uk. 36-37
  • Imechapishwa: 31/03/2024