Kuwafuatafuata watawala na viongozi wa ngazi mbalimbali serikali

Swali: Ni vipi yatafasiriwa maneno ya Salaf pindi waliposimanga kuingia kwenye majumba ya wafalme?

Jibu: Ni kwa yule anayewasifu na kukubaliana nao katika batili yao. Ni kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Baada yangu watakuongozeni watawala madhalimu. Yule atakayewasadikisha juu ya uwongo wao na akawasaidia dhuluma yao, hatokani nami, nami sitokani naye. Na yule asiyewasadikisha juu ya uwongo wao na asiwasaidia dhuluma yao, anatokana nami, nami natokana naye.”

Akiingia majumbani kwao kwa ajili ya kuwaelekeza, kuwashauri na kupunguza maovu yao, hivi ndivo inavotakikana. Lakini akiingia majumbani kwao kwa ajili ya kuwasaidia juu ya dhuluma na kuwasadikisha uwongo wao, haya ndio yanayosimangwa.

Vivyo hivyo imekuja katika Hadiyth:

“Asinifikishie yeyote kutoka kwa yeyote chochote.”

Hadiyth hii ni dhaifu na ndani yake kuna ujinga. Endapo itasihi, basi inafasiriwa juu ya kitu kisichowadhuru waislamu. Lakini ikiwa ni jambo linalowadhuru waislamu, ni lazima kumfikishia taarifa mtawala ili waislamu wawe makini. Hadiyth hii – ingawa ni dhaifu, kutokana na ujinga uliyomo – lakini izingatiwe maana yake. Maana yake ni sahihi. Waislamu wamfikishie mtawala taarifa kwa jambo lenye manufaa na wasimfikishie taarifa zenye madhara na hazina manufaa. Kwa ajili hii wakati Zayd bin Arqam alipomsikia ´Abdullaah bin Ubayy akizungumza vibaya katika baadhi ya safari zao kwa kusema:

“Hakika mtukufu zaidi atamtoa [katika mji] ambaye ni mdhalilifu.”

alimfikishia taarifa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bali Allaah aliteremsha Aayah ndani ya Qur-aan hali ya kumsadikisha.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/23221/على-ماذا-يحمل-ذم-الدخول-على-السلاطين
  • Imechapishwa: 28/11/2023