Swali: Je, inafaa kwa mwadhini kutoka nje ya msikiti baada ya kutoa adhaana kutokana na baadhi ya mahitaji yake kama kwa mfano alikuwa na wageni na anataka kuwaaga kisha arudi kabla ya kukimiwa swalah? Je, inafaa kwake kutoa adhaana bila kuwa na twahara kisha akatoka kwa ajili ya kutawadha?

Jibu: Inafaa kutoka nje ya msikiti baada ya kuadhini kutokana na haja iliyozuka kama mfano wa kutawadha au haja nyingine aliyotaja muulizaji akiwa atarejea kabla ya kukimu. Haijuzu kutoka nje baada ya adhaana kwa yule asiyetaka kurudi isipokuwa kutokana na udhuru unaokubalika katika Shari´ah. Hayo ni kutokana na yale yaliyothibiti kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) wakati alipomuona bwana mmoja ametoka nje ya msikiti baada ya adhaana akasema:

“Kuhusu huyu amemwasi Abul-Qaasim (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Wanazuoni wanaifasiri juu ya yule ambaye hana udhuru unaokubalika katika Shari´ah kwa ajili ya kutendea kazi dalili zote.

Inafaa kwa muislamu kuadhini pasi na kuwa na twahara kisha akajitwahirisha baada ya hapo. Lakini bora ni ile adhaana yake akiwa na twahara. Hayo ni kutokana na yale yaliyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Asiadhini isipokuwa aliyetawadha.”

Lakini hata hivyo cheni ya wapokezi wake ni dhaifu. Lakini kinachopata kufaidika kutoka hapo ni kwamba kutawadha ndio bora zaidi kukiwa na wepesi wa kufanya hivo. Vivyo hivyo kufanya Tayammum kwa ambaye ameshindwa kutawadha kutokana na maradhi au kukosa maji.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/338)
  • Imechapishwa: 18/09/2021