Kutamba ni kule kuondoa najisi. Hili ni jambo lisilokuwa na uhusiano na wudhuu’. Lau mtu atajisaidia haja ndogo au kubwa kishaakatamba kwa maji, baada ya hapo akaenda katika kazi zake na kukaingia wakati wa swalah, basi atatawadha kwa kuosha viungo vinne na hana haja ya kutamba tena. Kwa sababu kutamba ni kuondosha najisi. Pale ambapo najisi itaondoka hatorudi kuosha tena mara ya pili isipokuwa ikiwa kama najisi itakuwa imerudi mara nyingine.

Maoni sahihi ni kwamba lau atasahau kutamba kwa mawe kwa mujibu wa Shari’ah kisha akatawadha, wudhuu’ wake ni sahihi. Kwa sababu hakuna mafungamano kati ya kutamba na wudhuu’.

Ama ikiwa amepatwa na hadathi kubwa kama mfano wa janaba, ni lazima kwake kuoga. Alowe mwili wake mzima maji. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا

“Na mkiwa na janaba basi jitwaharisheni.” (05:06)

Humo kunaingia pia kusukutua na kupalizia. Kwa kuwa kusukutua na kupalizia ni sehemu ya uso. Hivyo ni wajibu kusafisha pua na kinywa kama jinsi ni wajibu kuosha paji la uso, mashavu na ndevu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/363)
  • Imechapishwa: 14/05/2023