Swali: Ni ipi hukumu ya kutamani kifo?

Jibu: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza mtu kutamani kifo kutokana na dhara lililompata. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Asitamani yeyote kifo kutokana na dhara lililompata. Ikiwa hana budi isipokuwa kufanya hivo, basi na aseme:

اللهُمَّ أَحْيِنِي مَا كَانَتِ الْحَيَاةُ خَيْرًا لِي، وَتَوَفَّنِي إِذَا كَانَتِ الْوَفَاةُ خَيْرًا لِي

“Ee Allaah! Nipe uhai muda wa kuwa uhai ni kheri kwangu. Na nifishe ikiwa kifo ni kheri kwangu.”[1]

Hadiyth haina lolote kuhusiana na maneno yake Maryam (Radhiya Allaahu ´anhaa):

لَيْتَنِي مِتُّ قَبْلَ هَـٰذَا وَكُنتُ نَسْيًا مَّنسِيًّا

”Laiti ningelikufa kabla ya haya na nikawa mwenye kusahaulika kabisa!”[2]

Huku sio kutamani kifo isipokuwa ni kutamani kama angelikuwa amekufa kabla ya tukio hili lililomtokea. Vivyo hivyo kuhusiana na maneno yake Yuusuf (´alayhis-Salaam):

تَوَفَّنِي مُسْلِمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ

“Nifishe nikiwa muislamu na unikutanishe na waja wema.”[3]

Haimaanishi kuwa anamwomba Allaah kifo. Isipokuwa anamwomba Allaah afe katika hali hii, kwa maana ya kwamba amfishe hali ya kuwa ni muislamu. Kwa hivyo hayapingani na makatazo yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya mtu kutamani kifo.

[1] al-Bukhaariy (5671) na Muslim (2680).

[2] 19:23

[3] 12:101

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/62-63)
  • Imechapishwa: 12/07/2026