Itambulikane kuwa mtu kuswali kabla ya kuingia wakati swalah haikubaliwi. Hata ikiwa mtu ataleta Takbiyrat-ul-Ihraam na kisha baada ya hapo wakati ukaingia, swalah haikubaliwi kwa vile ni faradhi. Kitu kilichowekewa wakati wake maalum hakisihi kikifanywa kabla ya kuingia kwa wakati wake. Ni kama mfano wa mwenye kufunga kabla ya kuingia Ramadhaan, hata kama itakuwa kwa siku moja kabla, swawm yake ya Ramadhaan haikubaliwi. Vivyo hivyo lau mtu ataleta Takbiyrat-ul-Ihraam kabla ya kuingia kwa wakati, swalah yake haikubaliwi kwa vile ni faradhi. Lakini hata hivyo ikiwa ni mjinga asiyejua, inakuwa ni yenye kupendeza na ni wajibu kwake kuirudi kuiswali tena hiyo faradhi. Kuhusiana na mtu akiswali baada ya kuingia kwa wakati, hilo halitoki katika hali mbili:

1 – Ima mtu akawa ni mwenye kupewa udhuru kutokana na ujinga, amesahau au amepitikiwa na usingizi. Huyu swalah yake inakubaliwa.

a) Mtu mjinga ni kama mfano wa asiyejua kuwa muda umeshaingia na umemalizika, huyu hakuna kitu juu yake. Pale atapojua [kuwa wakati umeshaingia] aswali na swalah yake inakubaliwa kwa kuwa ni mwenye kupewa udhuru.

b) Mwenye kusahau ni kama mfano wa mwenye kufanya kazi kubwa na ikamshughulisha akaghafilika mpaka wakati ukamalizika. Huyu anaiswali hata kama wakati utakuwa umeshamalizika.

c) Mtu mwenye kupitikiwa na usingizi. Lau mtu atalala na ameazimia kuamka wakati wa adhaana, lakini hata hivyo usingizi wake ukawa mzito na hakusikia adhaana na wala hakusikia alamu aliyoweka karibu na kichwa chake mpaka wakati ukatoka, huyu ataswali pale atapoamka. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesma:

“Mwenye kupitikiwa na usingizi au akaisahau swalah, basi aiswali pale atapoikumbuka. Haina kafara nyingine isipokuwa hiyo.”[1]

2 – Akachelewesha swalah kwa kukusudia bila ya udhuru wowote. Wanachuoni wote wamekubaliana kuwa mtu huyu ni mwenye kupata dhambi na ni mwenye kumuasi Allaah na Mtume Wake. Baadhi ya wanachuoni wengine wamesema kuwa mtu huyu anakufuru kufuru yenye kumtoa katika Uislamu.Wanachuoni wamekubaliana juu ya kwamba akichelewesha swalah mpaka ukatoka wakati wake, bila ya udhuru, ni mwenye kupata madhambi na ni mfanya maasi. Wako waliosema kuwa anakufuru. Lakini kikosi cha wanachuoni wengi – na haya ndio maoni sahihi – ni kwamba hakufuru. Katika hali hii wanachuoni wametofautiana tena lau ataiswali baada ya kuwa wakati wake umeshatoka na amefanya hivo kwa kukusudia pasina udhuru:

1 – Wako waliosema kuwa swalah yake inakubaliwa. Kwa kuwa amejirudi katika usawa na isitoshe ikiwa watu zinakubaliwa swalah zao baada ya wakati wake, basi vivyo hivyona mwenye kufanya hivo kwa kukusudia inakubaliwa.

2 – Wengine wakasema kuwa haikubaliwi.

Maoni sahihi ambayo yanasapotiwana dalili ni kwamba haikubaliwi. Akiitoa nje ya wakati wake kwa kukusudia, basi swalah yake haikubaliwi hata kama ataswali mara elfu moja. Hilo ni kutokana na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote mwenye kufanya kitendo kosichoafikiana na amri yetu, basi atarudishiwa mwenyewe.”[2]

Bi maana atarudishiwa na haikubaliwi na Allaah. Ikishakuwa ni yenye kurudishwa ina maana haikubaliwi.

Huyu ambaye ameitoa swalah nje ya wakati wake kwa kukusudia, akiiswali basi ameswali juu ya isiyokuwa amri ya Allaah na Mtume Wake. Hivyo haikubaliwi. Lakini ikiwa ana udhuru anapewa udhuru. Hivyo ndio maana Shari´ah imeamuamrisha kuiswali pale ambapo udhuru wake utakatika. Kuhusu mtu ambaye hana udhuru wowote, lau atabaki na kuswali mwaka mzima, swalah yake hii aliyoiswali nje ya wakati bila ya udhuru haitokubaliwa. Pamoja na hivyo lililo la wajibu kwake ni kutubu kwa Allaah, kujirekebisha, kukithirisha matendo mema na kuomba msamaha. Mwenye kutubu basi Allaah humsamehe.

[1]al-Bukhaariy (597) na Muslim (684).

[2] Muslim (1718).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/360-362)
  • Imechapishwa: 10/05/2023