Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

عن أبي سِروْعَة- بكسر السين المهملة وفتحها- عُقبةَ بن الحارث رضي الله عنه قَالَ: صَلَّيتُ وَرَاءَ النَّبيّ صلى الله عليه وسلم بالمَدِينَةِ العَصْرَ، فَسَلَّمَ ثُمَّ قَامَ مُسْرِعًا، فَتَخَطَّى رِقَابَ النَّاسِ إِلَى بعْضِ حُجَرِ نِسَائِهِ، فَفَزِعَ النَّاسُ مِنْ سُرْعَتِهِ، فَخَرَجَ عَلَيهمْ، فَرأى أنَّهمْ قَدْ عَجبُوا مِنْ سُرعَتهِ، قَالَ: ((ذَكَرتُ شَيئًا مِنْ تِبرٍ عِندَنَا فَكَرِهتُ أنْ يَحْبِسَنِي فَأمَرتُ بِقِسْمَتِهِ)). رواه البخاري.

وفي رواية لَهُ: ((كُنتُ خَلَّفتُ في البَيْتِ تِبرًا مِنَ الصَّدَقةِ فَكَرِهتُ أنْ أُبَيِّتَهُ)). ((التِّبْرُ))

88 – Abu Sirw’ah, ‘Uqbah bin al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anh) amesimulia:

”Niliswali nyuma ya Nabii (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) al-‘Aswr al-Madiynah. Akatoa salamu kisha akainuka haraka ambapo akawa anaziruka shingo za watu kuelekea katika baadhi ya vyumba vya wakeze. Watu wakashangaa kutokana na ile haraka yake. Akawatokezea na kuona kuwa wamemstajabu kwa ile haraka yake ambapo akawaambia: “Nilikumbuka kitu katika kipande cha dhahabu kilichokuwa kwetu, nikakichukua kisije kikanizuia, nikaamuru kigawanywe.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Nilikuwa nimeacha nyumbani kipande cha dhahabu cha Swadaqah ambapo nikachukia kisije kikapitiwa na usiku.”

MAELEZO

Katika Hadiyh hii kuna dalili juu ya kujuzu kupita kati ya shingo za watu baada tu ya kutoa salamu ya swalah. Hili linafaa na khaswa ikiwa kuna haja. Hilo ni kwa sababu watu baada ya kutoa salamu hawana haja ya kubaki mahala pao. Wanapata ruhusa ya kutoka. Hili ni tofauti na kupita kati ya shingo za watu kabla ya swalah, ni jambo ambalo limekatazwa kwa sababu linawaudhi watu. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisimamisha Khutbah yake siku ya ijumaa pindi walipomuona mtu anapita kati ya shingo za watu, akamwambia:

“Hebu kaa chini. Kwani hakika umeudhi.”[1]

[1] Abu Daawuud (1118).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (02/22)
  • Imechapishwa: 11/10/2023