Haijuzu kwa mtu kumuasi mtawala katika yasiyokuwa maasi na akasema kuwa hii sio dini. Wapo baadhi ya wajinga mtawala anapoweka nidhamu isiyoenda kinyume na Shari´ah wanasema sio lazima kwetu kutekeleza nidhamu hii kwa kuwa sio Shari´ah na haipatikani katika Qur-aan wala Sunnah. Huu ni ujinga. Bali tunasema kutekeleza nidhamu hii ni jambo lipo ndani ya Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.” (04:59)

Vilevile imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth nyingi ambapo ameamrisha kumtii mtawala na moja wapo ni Hadiyth hii. Hivyo kumtii mtawala katika nidhamu walizoweka ambazo haziendi kinyume na Shari´ah, ni miongoni mwa yale aliyoamrisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ingelikuwa haifai kumtii mtawala isipokuwa katika yale tu ambayo Allaah na Mtume Wake wameamrisha, basi kumtii mtawala kusingelikuwa na faida yoyote. Kwa sababu kumtii Allaah (Ta´ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni jambo limeamrishwa, ni mamoja ikiwa jambo hilo limeamrishwa na mtawala au hakuliamrisha.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/536-537)