12. Du´aa ambayo mara nyingi Mtume akiiomba

55 – Abu Mu´aawiyah ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Abu Sufyaan, kutoka kwa Anas aliyesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikithirisha kusema:

يا مقلب القلوب ثبت قلبي على دينك

“Ee mwenye kuzigeuza nyoyo! Uthibitishe moyo wangu juu ya dini Yako.”

Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tumekuamini, na yale uliyokuja nayo; je, unachelea kwetu?” Akasema: “Ndio. Hakika nyoyo ziko kati ya vidole viwili katika vidole vya Mwingi wa huruma (´Azza wa Jall). Anazigeuza.”[1]

56 – Mu´aadh bin Mu´aadh ametuhadithia: Abu Ka´b mzee wa hariri ametueleza: Shihr bin Hawshab ametueleza:

“Nilisema kumwambia Umm Salamah: “Ee mama wa waumini, ni ipi du´aa aliyokuwa akiomba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapokuwa kwako?” Akasema: “Du´aa yake nyingi ilikuwa:

يا مقلب القلوب ثبت قلبي على دينك

“Ee mwenye kuzigeuza nyoyo! Uthibitishe moyo wangu juu ya dini Yako.”

Akasema: “Ee Umm Salamah! Hakuna mwanadamu yeyote isipokuwa moyo wake uko kati ya vidole viwili katika vidole vya Mwingi wa huruma. Akitaka anaunyoosha, na akitaka anaupindisha.”

57 – Yaziyd bin Haaruun ametuhadithia: Hammaam bin Yahyaa ametueleza, kutoka kwa ´Aliy bin Zayd, kutoka kwa Umm Muhammad, kutoka kwa ´Aaishah ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema:

يا مقلب القلوب ثبت قلبي على دينك

“Ee mwenye kuzigeuza nyoyo! Uthibitishe moyo wangu juu ya dini Yako.”

Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah, hakika wewe unaomba du´aa hii?” Akasema: “Ee ´Aaishah, hujui kuwa moyo wa mwanadamu uko kati ya vidole viwili vya Allaah? Akitaka kuipindua katika uongofu, basi anaipindua, na akitaka kuipindua katika upotofu, basi anaipindua.”

[1] at-Tirmidhiy (3522) na Ibn Maajah (3834) Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti za Muslim. Ahmad (3/257) ameipokea kupitia njia nyingine kutoka kwa al-A´mash, na at-Tirmidhiy, kupitia kwa Abu Mu´aawiyah, ambaye amesema kuwa Hadiyth ni nzuri. Amezidisha katika nyingine ”Anaupindisha anavyotaka.”

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 28
  • Imechapishwa: 10/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy